Watoto wa mitaani wanavyobakwa Sumbawanga

  • Baadhi ya watoto wa mitaani wanakiri kufanyiwa unyama huo na watu mbalimbali.Vitendo hivyo hufanywa kwa siri kubwa, kutokana na ukweli kwamba watoto hao katika hali ya kujilinda wameaanzisha mkakati maalum kupambana na watu wanaolawiti na kuwabaka watoto.

Watoto kulawitiwa ili wapate hifadhi ya kulala au kupewa chakula kizuri ni sehemu ya maisha ya baadhi ya watoto waishio mitaani mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.
Hii ni siri kubwa ambayo imejificha miongoni mwao, ili uweze kupata siri hii inakulazimu lazima ujenge uhusiano wa karibu na wa muda mrefu na watoto hao.
Watuhumiwa wakubwa wa kuwaingilia kinyume na maumbile watoto hao ni baadhi ya walinzi wanaolinda katika maduka ya biashara na vijana waliowazidi umri; vitendo hivyo vinaonekana  kushika kasi.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na Mwandishi wa makala haya kwa miezi kadhaa, umebaini kuwa vitendo vichafu vimesababisha baadhi yao kuathirika kisaikolojia hivyo kujikuta wakiona jambo hilo ni la kawaida na hulifurahia.
Watoto hao hufanyiwa vitendo hivyo hasa kipindi cha masika ambapo mvua huwa zinanyesha, maeneo ambayo hupendelea kulala nyakati hizo kwenye majumba ambayo ujenzi wake haujamalizika (Mapagala) huwa yanavuja maji ya mvua hivyo hulazimika kuyazikimbia kujisalimisha popote.
Watoto wa mitaani
Baadhi ya watoto wa mitaani waliozungumza na mwandishi walikiri kwamba ni kweli kuna tabia hiyo lakini ni kwa usiri mkubwa kwani iwapo itabainika mtu anamlawiti mtoto mwenzao huwa wanapambana naye.
“Unajua sisi tunawasaidia walinzi katika malindo yao nyakati za usiku, tulishakubaliana kama kuna mwenzetu analawitiwa na anakubali tutamtenga.
Wapo watoto wawili tayari tumewatenga katika kundi letu kwa tabia ya kupenda kulawitiwa, sasa kama wapo wengine tukiwafahamu nao tunawatenga hata wakipata matatizo hatuwezi kuwasaidia” mtoto mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Jose (siyo jina lake halisi).
Naye mtoto aitwaye Juma anasema kuwa kinachowaponza watoto wengine ni tamaa na sio hifadhi ya kulala pekee kwani wapo watoto ambao wamezitoroka familia zao kwa kisingizio cha ugumu wa maisha na kukimbilia mitaani kufanya kazi ya kuombaomba ambapo wamekuwa wakidanganyika kwa vyakula kama Chips na pombe katika baa za usiku.
“Sisi wengine tupo huku mitaani kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kipato duni cha familia zetu, malezi mabaya kama vile kulelewa na kina mama wa kambo ambao ni chanzo matatizo kwa sehemu kubwa lakini sio sababu ya kukubali kulawitiwa.
Ila wapo wale wanaopenda pombe na chips ndio wanajikuta wakishawishiwa na sio tu na walinzi lakini pia hata baadhi ya watu ambao hutumia kisingizio cha ulevi wa pombe ili kufanya vitendo hivyo,” anasema mtoto Maiko (siyo jina lake halisi).

Socials