ULANGUZI WA TIKETI WAPAMBA MOTO UBUNGO

Kama unavyoona, hapa hali ya usafiri ni mbaya magari hakuna, nauli ya kwenda Iringa imefika Sh50,000. Ni hatari kubwa kwa wasafiri. Dar es Salaam. Nauli za mabasi ya mikoani na nchi jirani zimeendelea kupanda, na sasa Mikoa ya Iringa na Tanga nayo imeguswa na ongezeko hilo.
Mbali na nauli hizo kuzidi kupanda, hali ya usafiri nayo imeendelea kuwa mbaya na kuleta usumbufu mkubwa wananchi kutokana na idadi ndogo ya mabasi katika Kituo Kikuu cha Ubungo (UBT).
Ongezeko la nauli katika Mikoa ya Iringa na Tanga hasa kwenye Wilaya ya Lushoto, lilibainika jana wakati maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) walipofanya ukaguzi UBT.
Mwananchi jana ilifika katika kituo hicho na kushuhudia idadi kubwa ya watu waliokuwa wakitafuta usafiri wa kwenda mikoani.
Wakizungumza kituoni hapo baadhi ya abiria walidai kuwa baada ya hali kuwa mbaya katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, sasa imehamia Mikoa ya Iringa na Tanga.
Nauli za Arusha na Kilimanjaro zimepanda kufikia Sh35,000, Sh40,000 na Sh50,000 badala ya nauli ya kawaida ya Sh23,000 na 25,000 kwa mabasi ya kawaida.
Nauli ya Iringa nauli imepanda kutoka Sh18,000 na Sh20,000 hadi kufikia Sh40,000 na Sh50,000. Tanga imepanda kutoka Sh10,000 na Sh12,000 hadi kufikia Sh20,000.
Mmoja ya abiria aliyejitambulisha kwa jina la Subira Ramadhani aliyekuwa akisafiri kwenda Iringa, alisema nauli imefika Sh40,000 na Sh50,000 kutoka Sh18,000 na Sh20,000.
“Kama unavyoona, hapa hali ya usafiri ni mbaya magari hakuna, nauli ya kwenda Iringa imefika Sh50,000. Ni hatari kubwa kwa wasafiri,” alisema Ramadhani.
Ofisa kutoka Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Gelvas Rutabuzinda alikiri kuwa hali bado ni mbaya kutokana na baadhi ya mabasi kupandisha nauli.
“Kama unavyona bado hali siyo shwari, nauli zinaendelea kupanda abiria wanalubuniwa,” aliongeza Rutabuzinda.
Naye Ofisa Leseni wa Sumatra Sebasitian Lohay alisema mpaka sasa mabasi zaidi ya 20 yametozwa faini kwa makosa ya kupandisha nauli.

Socials