Wagombea urais CCM wafungukakia Kauli ya Rais Kikwete Aliyosema Urais ni Kazi Ngumu na ya Kadhia


Siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema kuwa nafasi hiyo ni kadhia na kazi ngumu, baadhi ya wanasiasa waliotangaza nia ya kuwania nafasi hiyo wamesema wanafahamu changamoto hizo na kwamba kauli hiyo inazidi kuwapa nguvu na hamasa ya kuendelea na mchakato huo.

Wiki iliyopita, Rais Kikwete akiwa Marekani, wakati akihutubia kwenye taasisi ya Wood Wilson International Center for Scholars alielezea mafanikio na changamoto alizokumbana nazo wakati wa uongozi wake wa miaka 10 unaomalizika Oktoba, mwaka huu na kusema:

“Wakati unaingia Ikulu unakuwa na shauku kubwa sana pamoja na furaha ya ushindi, lakini hakika urais ni kadhia kubwa. Ukipata fursa ya kuwa rais kwa awamu mbili kama mimi nadhani zinatosha kabisa. Nimefanya mengi kwa nchi yangu atakayekuja ataendeleza nilipoishia.”

Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja wakati makada wa CCM wakipigana vikumbo kuwania urais.

January Makamba:
"Nilitangaza nia hiyo huku nikiwa nafahamu kwa asilimia 100 uzito wa jambo hilo... kufahamu changamoto hizo ndiyo moja ya vitu vilivyonisukuma kuchukua uamuzi huo,” alisema.

Sumaye:
“Kama mtu ameamua kuwania nafasi hiyo ina maana anafahamu anachokitaka. Tunajua ziko changamoto na namna ya kukabiliana nazo kwa hiyo hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi.”

Dk Kigwangalla alisema:
“Kauli kama hiyo haiwezi kumvunja mtu moyo, ari itabaki palepale tu kwa aliyetangaza nia. Aliyetangaza nia anataka kutoa utumishi wake kwa nchi yake kama mimi.”

Socials