WABUNGE WATAKA TUME KUCHUNGUZA MASHINE ZA TRA 'EFD'

Wafanyabiashara wa Kariakoo, Dar es Salaam walifunga maduka, Novemba 18, mwaka huu wakipinga utaratibu mpya wa TRA wa kutoza kodi kwa kutumia mashine hizo.

Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara imependekeza kuundwa kwa tume huru kuchunguza uhalali wa bei za mashine za risiti za kielektroniki (EFD) kutokana na malalamiko ya wafanyabiashara nchi nzima.
Kamati hiyo imesema endapo itabainika kulikuwa na udanganyifu wa bei, wahusika wote walioshiriki katika mchakato wa kununua mashine hizo basi wachukuliwe hatua kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi ya Umma.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mahmoud Mgimwa alisema jana kwamba endapo kutabainika kuwapo udanganyifu, Serikali iondoe kodi ya vifaa hivyo na tume ipendekeze bei mpya.
Akiwasilisha taarifa ya kamati yake, Mgimwa alisema taarifa walizopewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zinaonyesha bei ya mashine hizo ni kati ya Sh600,000 na Sh778,377.
“Gharama za mashine hizo zinajumuisha gharama za ubadilishaji wa fedha yaani `exchange rate’, kodi ya ushuru wa forodha, gharama za usambazaji na uendeshaji wa biashara,” alisema.
Alisema tatizo la matumizi ya mashine za EFD limekuwa kubwa na kusababisha maduka kufungwa kutokana na migomo katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Morogoro.
“Wafanyabiashara wanalalamikia bei kubwa ya mashine hizo ukilinganisha na bei ya kununulia mashine hizo katika nchi za China na Falme za Kiarabu (UAE) na zinaandika bei za juu kuliko bei halisi,” alisema.
Akichangia taarifa ya kamati hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Pauline Gikul aliunga mkono pendekezo hilo la kamati na kuorodhesha matatizo mengine ya mashine hizo.
Alisema mbali na kwamba bei ya mashine hizo ni kubwa, lakini bunda moja la karatasi huuzwa kwa Sh10,000 na hutoa risiti 20 tu na kwamba mfanyabiashara hawezi kumuuzia mtu mwingine mashine hiyo.
“Mbali na gharama zote hizo bado mfanyabiashara anatakiwa kulipa Sh135,000 kwa mwaka kama gharama za ukaguzi na wanatozwa Sh50,000 kwa kila matengenezo mashine inapoharibika,” alisema.
Mbunge huyo alisema agizo la TRA kutaka wafanyabiashara wote kununua na kutumia mashine hizo lisitishwe kwa muda wakati tume hiyo itakayoundwa itakapokuwa ikichunguza suala hilo.

Socials