OKWI AVURUGA MTAA WA MSIMBAZI

Dar es Salaam. Mamia ya mashabiki wa Simba jana walikusanyika makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam wakitaka kujua ukweli kuhusu uhamisho wa Emmanuel Okwi kwenda Yanga.
Hali hiyo ilisababisha msongamano wa magari kwa muda katika Barabara ya Msimbazi wakati mashabiki hao wakisubiri kuonana na viongozi wao.
Mmoja wa mashabiki hao aliyejitambulisha kwa jina la Hamas Ibrahimu aliliambia gazeti hili kuwa sasa umefika wakati wa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Rage kuwajibika kabla ya kuwajibishwa.
“Sasa hakuna haja ya kumtetea tena Rage anachotakiwa ni yeye mwenyewe kuwajibika kwa kuachia ngazi kwa sababu ametudanganya sana na leo hii Okwi ametua Yanga tena kwa wepesi kabisa bila ya kulipwa fedha zetu na  Etoile du Sahel,” alisema Ibrahimu.
Naye mwenyekiti wa Simba, Aden Rage amelitaka Shirikisho la Soka la Dunia (Fifa) kuingilia kati ili klabu yake ilipwe Dola 300,000 za mauzo ya mshambuliaji Emmanuel Okwi.
Rage alisema jana kuwa, haelewi ni kwa misingi gani iliyoiruhusu klabu ya SC Villa, Uganda kumuuza Okwi Yanga ambaye alikuwa akitumia leseni maalumu ya miezi sita iliyotolewa na Fifa.
“Ieleweke kuwa Simba haimpiganii Okwi kwani si mchezaji wetu tulishamuuza, lakini tunadai malipo yetu,” alisema Rage
Alidai kuwa hajui kama Fifa ilivunja mkataba wa Etoile na Okwi ambaye alikuwa analalamikia kutolipwa fedha zake za mkataba na mshahara.
“Ni lazima haki yetu ilipwe hata ikitokea nini, Saleh na Okwi watajuana wao,” alisema na kuongeza: “Mchezaji ukishamuuza si wako tena na huma mamlaka naye.”

Socials