Kinyume na matarajio ya wengi, mradi wa Upanuzi wa Barabara ya Morogoro, kilomita 21 kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Kimara umekuwa kero kubwa kwa wananchi wanaotumia vyombo vya usafiri kupitia katika barabara hiyo. Tangu kuanza kwa mradi huo yapata miaka miwili hivi iliyopita, tumeshuhudia wananchi wengi wanaotumia barabara hiyo wakionyesha kuchoshwa na adha wanazozipata kutokana na misururu mirefu ya magari barabarani.
Madereva na abiria wanaotumia barabara hiyo na nyingine nyingi zinazokatiza kutoka sehemu mbalimbali za jiji sasa wanauona upanuzi wa barabara hiyo kama laana badala ya faraja. Wapo wanaosema mradi huo ni wa ovyo. Mbunge mmoja alisema bungeni mjini Dodoma hivi karibuni kwamba misururu ya magari ambayo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na mradi huo ni janga la kitaifa.
Kauli za aina hiyo ni kielelezo tosha kwamba watumiaji wa barabara hiyo wamechoshwa na adha zinazosababishwa na upanuzi wa barabara hiyo, ambao unaonekana kutokuwa na mwelekeo na usimamizi makini. Siyo jambo la kufikirika hata kidogo kwamba inachukua zaidi ya saa tatu au nne kutoka katikati ya Jiji hadi Kimara au kutoka Tazara hadi Mwenge au kutoka makutano ya Barabara za Nyerere na Kawawa hadi Kawe kupitia Magomeni. Umuhimu wa Barabara ya Morogoro kwa wasafiri na vyombo vya usafiri ni mkubwa mno kwa sababu ni kiunganishi kikubwa cha barabara nyingi, zikiwamo za Ali Hassan Mwinyi na Kilwa zinazoingia na kutoka jijini kama ilivyo Barabara ya Morogoro.
Zipo taarifa nyingi zinazoeleza jinsi kadhia ya msongamano wa magari jijini ulivyosababisha migogoro ya kifamilia na katika sehemu za kazi. Kuchelewa sana kufika nyumbani kutoka kazini kumeelezwa kusababisha ugomvi wa mume na mke kwa kutuhumiana kukosa uaminifu, kama ilivyo kwa wafanyakazi wanaotuhumiwa na waajiri wao kwa uzembe na hujuma kutokana na kuchelewa kazini kwa ‘kisingizio cha foleni barabarani’.
Pamoja na athari hizo za kijamii, zipo athari kubwa za kiuchumi. Msongamano wa magari baada ya kuanza mradi huo wa Barabara ya Morogoro unakadiriwa kuwa zaidi ya Sh4 bilioni kila siku zikiwa ni gharama za petroli na dizeli, mbali na wafanyakazi na wafanyabiashara kupoteza muda mrefu (man hours) njiani kabla ya kufika katika sehemu zao za kazi.
Lakini nani anajali? Inaonekana kwamba TANROADS inayopaswa kuisimamia Kampuni ya Strabag inayopanua barabara hiyo imeshindwa kufanya hivyo. Matokeo yake ni kwamba kampuni hiyo inafanya itakavyo kwa kufunga michepuo ya barabara zinazoingia au kutoka katika Barabara ya Morogoro pasipo kutoa taarifa wala kuonyesha alama zozote. Hicho ndicho chanzo cha vurugu na sintofahamu kubwa, kwani magari yanashindwa kwenda mbele ama kurudi nyuma, hivyo kusababisha msongamano mkubwa barabarani.
Maswali bado yanaulizwa kama kweli mradi huo ukikamilika utaweza kupunguza msongamano wa magari jijini, kwani tathmini nyingi zimeonyesha kwamba ni barabara za juu (fly-overs) na usafiri wa reli ndiyo pekee unaoweza kupunguza au kumaliza msongamano wa magari barabarani. Tunaitaka Serikali, kupitia TANROADS iisimamie Kampuni ya Strabag isifanye kazi yake kihuni kama inavyofanya hivi sasa. Ikumbukwe kwamba Jiji la Dar es Salaam ndiyo mhimili mkubwa wa uchumi wa nchi yetu. Kinachofanywa na Strabag ni sawa na kuhujumu uchumi wetu.