Athari ya vyuo vikuu kutojitangaza kwa jamii


Wanafunzi wengi hujikuta njia panda baada ya kuingia chuo kikuu. Baadhi inawabidi kubadili fani walizozichagua wenyewe, huku wengine wakitamani kufanya hivyo lakini kwa sababu mbalimbali wanashindwa.
Kwa sababu hiyo wako wanaojikuta wakihitimu katika fani wasizozipenda, matokeo yake huishia kufanya kazi wasizozipenda ama kukimbilia fani ambazo hawakusomea.
Uzoefu unaonyesha hali hii siyo ngeni nchini, huku kila upande kuanzia wanafunzi wenyewe, shule, wazazi na vyuo vikuu ukielezwa kuwa na mchango katika kuikuza hali hiyo.
Ilivyo ni kuwa hadi wanafunzi wanamaliza kidato cha sita, siyo wazazi au walimu shuleni wanaokaa na wanafunzi na kutafakari hatima kuhusu kuendelea na elimu ya juu.
Kwa sababu hii, baadhi ya wanafunzi wanashindwa kujua wasome nini na wapi pale yanapotoka matokeo na kubaini kuwa wamefaulu.
Wajibu wa vyuo kujitangaza
Udhaifu huu hauishii kwa walimu na wanafunzi wao shuleni, taasisi za elimu ya juu nazo hazina budi kubeba mzigo wa lawama, kwani nazo zinatajwa kwa kutokuwa na utaratibu wa kujitangaza kwa wanafunzi.
Matokeo yake pamoja na umahiri wa vyuo katika kufundisha baadhi ya kozi, jamii wakiwamo waajiri wanashindwa kujua chuo kipi kinafundisha nini?
Emilia Mkosamali ana ushuhuda mzuri wa namna baadhi ya waajiri wanavyokataa wanafunzi kufanya mazoezi ya vitendo katika ofisi zao kwa hoja kuwa hawajui kama kozi wanazoomba kufanyia mafunzo zinazofudishwa katika vyuo vyao.
Yeye ni miongoni mwa wanafunzi wanaosoma fani ya Rasilimali Watu (Human Resources – HR) katika Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco), waliopata wakati mgumu kupata mahala pa kujifunza kwa vitendo kama sehemu ya utekelezaji wa mtalaa.
Anasema kuwa, walipokuwa wakienda kwenye ofisi nyingi waliambiwa kuwa chuo chao hakifundishi fani hiyo, jambo analosema lilisababisha baadhi ya wanafunzi kutopata maeneo ya kufanya mafunzo hayo.
“Tulikuwa tunaambiwa Tumaini hawafundishi HR, wengine walipata sehemu ya mazoezi (mafunzo kwa vitendo) wakiwa tayari wamechelewa na wengine wengi tu hawakupata sehemu ya kufanyia mazoezi,” anaeleza.

Socials