TAARIFA ZA HABARI ZA TANZANIA HAZINA MVUTO KABISA JAMANI...BADILIKENI





Nilishaliongelea hilo kwenye post zilizopita nikilinganisha na Habari za TV za Kenya....sasa Bongo5 nao wameliongelea swala hilo kama ifuatavyo:

"Habari nyingi kwenye TV za kibongo hazina mvuto. Unaweza kufurahia kuangalia habari labda kama siku hiyo kuna ajali kubwa imetokea, bungeni kumeumana ama siku Barack Obama akirudi tena Bongo. Kusipokuwa na matukio ya kuvutia yaliyopo tayari, taarifa za habari kwenye TV zetu zinaboa si kidogo.
Watakujazia habari za mikutano, semina, warsha na mikutano na waandishi wa habari ambazo hazivutii hata chembe. Zinaweza kuwa na vigezo vya kuitwa ‘news’ lakini hizi si habari unazoweza kuziona kwenye TV za watu wanaojielewa. Hizi ni habari za kupoteza muda tu na wala hazina ‘impact’ yoyote kwa wananchi.
Nafahamu mazingira ya kufanya kazi kwenye TV za Tanzania na ninalo jibu la uhakika la kwanini habari za semina, warsha au press conference ndizo zinazotawala line-up ya habari kwenye vituo vyetu. Sababu kubwa ni kwamba waandishi wengi wa habari wanalipwa ujira mdogo mno na hivyo ili kujikimu kimaisha inabidi wafanye zaidi story za warsha na mikutano ambazo huwapa posho za hapa na pale.
Hiyo ina maana kuwa waandishi wengi wa habari hawana muda wa kuandika habari za kuvutia zinazohitaji ubunifu zaidi, muda wa kutosha na ‘mnuso wa habari’ (nose for news). Wamiliki wa vyombo vya habari wanahitaji kuwekeza zaidi katika kuwalipa vizuri waandishi wanaokusanya habari zao, kuwa na usafiri wa kuaminika na kuwa na wahariri wabunifu wenye uwezo wa kujua habari zenye mvuto, zenye impact na zilizoandikwa kwa kina.
Taarifa za habari pia zinatakiwa kuhusisha wataalam ama wachambuzi wa masuala mbalimbali kutilia mkazo ripoti husika. Mashirika makubwa ya habari ya kimataifa hupenda kutumiza ‘contributors’ mbalimbali ambao huhusika katika uchambuzi wa masuala ya siasa, biashara na uchumi, masuala ya jamii pamoja na michezo na burudani.
Kwa kutumia watu hawa, habari hupanuliwa zaidi na kuzungumzwa katika mtazamo mpana.
Kwa mfano, weekend hii Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, amedai kuwa bara la Afrika halimtendei haki Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kama mtu muhimu kwenye harakati za ukombozi wa Afrika kutoka kwa wakoloni. Hii ni habari ambayo inaweza kuripotiwa kwenye taarifa za habari katika TV za Tanzania kwa kuichambua zaidi kwa kuhusisha wazee na viongozi wa zamani watakaotoa maoni yao kutokana na kauli hii, viongozi wa juu wa Tanzania na hata wasomi wa vyuo vikuu kuipa wigo zaidi.
Kwa ufupi, matatizo makubwa kwenye taarifa za habari kwenye vituo vyetu vya runinga ni pamoja na:
Habari nyingi hazivutii
Wasomaji wengi wa habari hawana mvuto na hawavalishwi vizuri
Muonekano na uwasilishaji wa habari ni wa kawaida
Hakuna habari za kina na zenye uchambuzi
Habari si za kutafuta, nyingi ni za matukio ya kuandaliwa
Hakuna matumizi ya wataalam katika fani mbalimbali
Uandishi wa script hautumii maneno yenye kuvuta usikivu wa watu au matumizi ya lugha ya macho
Matumizi ya ripota wanaotumia simu za mkononi
Wasomaji wa habari hawategenezwi kuwa ‘TV personalities’ kama ilivyo Kenya ambako wamezaliwa watu maarufu na wenye ushawishi wakiwemo Julie Gichuru, Kanze Dena na Lulu Hassan au Swaleh Mdoe wa Citizen TV au Larry Madowo wa NTV na wengine
Habari zinakuwa serious mno na kusahau upande wa ‘humor’
Uandishi wa habari unachukuliwa kama taaluma kupitiliza na kusahau kuwa uandishi pia ni sanaa inayohitaji ubunifu kama uandishi wa vitabu au utunzi wa mashairi yenye mvuto
Waandishi wa habari na maripota wa TV ambao wako chini ya wahariri, wanatakiwa kuanza kufikiria nje ya box na kutafuta habari za maana na kuondokana na uandishi uliozoeleka wa‘Madiwani wa kata ya ‘Mti Mkavu’ wametakiwa kuwa waadilifu katika kazi yao’ ‘Ama mbunge wa Kilimabubu ameweka jiwe la msingi kwenye shule ya Mnazi Mchungu’.
Watazame aina ya habari wenzetu huziandika ambazo huwa na mvuto, zimechambuliwa vizuri, zimetumia vyanzo vya kutosha na uandishi wa script wenye maneno matamu"
Bongo5

Socials