HOFU YA MAFURIKO: MTOTO MLEMAVU AFUNGIWA DARINI MIEZI MINNE MTWARA






Mtwara. Mtoto Abdul Mohamedi (13) ambaye ni mlemavu wa viungo, amelazimika kuishi darini kwa miezi minne mfululizo kukwepa kudhuriwa na mafuriko kutokana mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mjini Mtwara.
Bibi wa mtoto huyo anayeishi Mtaa wa Magomeni Mbezi, Zainabu Lipuga (70), alisema jana kuwa alimpandisha darini mjukuu wake Novemba mwaka jana baada ya mafuriko yaliyotekea kipindi hicho.


Kushushwa kwa mtoto huyo kumekuja baada ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) Manispaa ya Mtwara Mikindani, kumtembelea Lipunga kwa lengo la kumjengea nyumba imara kutokana na kuishi katika mazingira hatarishi.
“Nilipoona mvua zinanyesha nikaona bora nimnusuru mjukuu wangu asisombwe na mafuriko kwa vile sina nguvu za kuweza kumpandisha na kumteremsha mara kwa mara,” alisema Lipuga na kuongeza:
“Mjukuu wangu ni mlemavu hawezi hata kukaa, katika kipindi chote hicho amekuwa akilala tu, najua anateseka sana hasa ukizingatia umbali wa dari na paa la bati ni karibu sana wakati wa jua kali anaumia sana ila sina jinsi.”
Alisema baba wa mtoto huyo ambaye ni mwanaye hajulikani alipo na kwamba jukumu la kumlea limeachwa mikononi mwake bila msaada.
Mjumbe wa umoja huo, Mwanahamisi Hamisi alisema chama chake kimeguswa na hali hiyo, hivyo kimeamua kumuondoa katika nyumba yenye miundombinu duni.


“Milango ipo wazi kwa wadau wengine kumsaidia bibi huyu ili aweze kuishi vizuri na mjukuu wake...inatia huruma yule mtoto anaathirika sana na jua kali kule darini, anahitaji kusaidiwa,” alisema Mwanahamisi.
Hata hivyo, wakati huo, manispaa hiyo ilikumbwa na mafuriko Januari mwaka huu.
Zaidi ya nyumba 200 zilizingirwa na maji kusababisha hasara kwa wananchi ikiwamo kuharibika mali zao zikiwamo nguo na vyakula.Katika janga hilo, hakuna mtu aliyeripotiwa kupoteza maisha.

KWA ZINGINE KALI BOFYA HAPA

Socials