Unyama Mkubwa: Mtoto Afungwa Minyororo Miezi Minne Kwa Mganga wa Kienyeji Kisa Deni la Matibabu
MATUKIO ya ukatili dhidi ya watoto, bado yameendelea kushika kasi kwenye maeneo mbalimbali nchini ambapo katika Mkoa wa Simiyu, mtoto mwenye umri wa miaka 17 (jina tunalihifadhi), mkazi wa Bariadi Mjini na mwanafunzi wa Shule ya Msingi Bariadi, amejikuta akifungwa minyororo mikononi na miguuni kwa miezi minne nyumbani kwa mganga wa kienyeji.
Mganga huyo amefahamika kwa jina la Mdeli Msanja ambaye aliamua kufanya ukatili huo baada ya wazazi wa mtoto huyo ambaye anamatatizo ya akili, kushindwa kumlipa pesa za matibabu.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Charles Mkumbo, alisema wazazi wa mtoto huyo walikubaliana na mganga huyo kumlipa sh. 260,000 kama mtoto wao atapatiwa matibabu na kupona.
“Pamoja na wazazi kukubaliana na mganga husika, hali ya mtoto haikuweza kubadilika wala kupata unafuu hivyo waliomba kumchukua mtoto wao kitendo ambacho kilipingwa na mganga kwa madai ya kutolipwa pesa zake ambazo walikubaliana,” alisema.
Alisema mganga huyo aliamua kumchukua mtoto huyo na kumfungia chumbani kwake kwa minyororo miguuni na mikononi kwa kipindi cha miezi minne akidai pesa zake na kuwapa wakati mgumu wazazi wake.
Kutokana na msimamo wa mganga huyo, mama mzazi wa mtoto huyo Malita James (46), alilazimika kwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Bariadi kuhusu mateso anayoyapata mwanaye kwa mganga.
“Polisi walishirikiana na Dawati la Jinsia kufanya uchunguzi wa tukio hili na walipofika kwa mganga, walimkuta akiwa amemfunga minyororo miguuni na mikononi,” alisema Kamanda Mkumbo.
Aliongeza kuwa, polisi walimkamata mganga huyo ambaye hakuwa na kibali cha kutoa tiba za asili, pia alikamatwa na nyara za Serikali ambazo ni pembe moja ya swala na mikia miwili ya nyumbu ambapo uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani.