VALENTINE'S DAY...AFUMANIWA, APIGWA, AZIMIA

Stori: Issa Mnally
SIMULIZI ya mrembo mmoja ambaye jina lake halikupatikana mara moja inatia majonzi na huzuni lakini habari mbaya zaidi ni kwamba alifumaniwa na mwanaume wa mtu, katikati ya shamrashamra za Sikukuu ya Wapendanao ‘Valentine’s Day’, akapewa kichapo hadi akazimia, Ijumaa Wikienda linakupa zaidi.
Mrembo aliyefumaniwa akipatiwa huduma ya kwanza baada ya kuzimia.
Tukio hilo lililovuta hisia za watu wengi, lilitokea Februari 14, mwaka huu, katika ukumbi mmoja wa ‘kulia bata’ uliopo Temeke jijini Dar es Salaam.
HARUFU YA KASHESHE
Awali, paparazi wetu aliyekuwa akijivinjari ukumbini humo akiwa na njaa ya habari, alimuona dada huyo akiwa na mwanaume mmoja mtanashati wakiwa wamekaa chobingo wakionekana kama vile ni mke na mume halali.
Wakiwa wamejiachia huku wakifurahia sikukuu hiyo ambayo kwa hapa Bongo imegeuzwa maana yake na kufanywa kuwa siku ya ngono, kamera ya Ijumaa Wikienda, iliamua kutulia kwa muda na kuwafuatilia.
 Wawili hao walikuwa kivutio kikubwa miongoni mwa wapendanao waliokuwemo ukumbini humo hasa kwa namna walivyovalia mavazi yao na kupendeza.
Mrembo akiwa amezimia baada ya kipigo.
RANGI NYEKUNDU
Katika kile kilichoonekana mrembo huyo alikuwa amepania sikukuu hiyo, alikuwa amevalia sketi na blauzi nyekundu, zenye ‘material’ ya bazee na jamaa naye akiwa ametupia jinzi la bluu na shati rangi ya damu ya mzee.
Wakiwa wanaendelea na stori za hapa na pale huku wakionekana kuwa wamekolea kwa kinywaji, dada mmoja alipita eneo lile na kusimama kwa muda mrefu akiwakazia macho, jambo lililomfanya paparazi wetu kuachana na mambo mengine na kusubiria kitakachotokea.
TIMBWILI
Haikuchukua hata dakika tano, yule dada alirudi akiwa na kampani yake, huku mwanamke mmoja ambaye alijitaja kuwa ni mke wa njemba yule akimvamia yule dada na kuanza kumpa kichapo.
“Nimekuvumilia sana wewe malaya, kwa nini unaniharibia maisha yangu? Mume wangu hatulii nyumbani, mi nahangaika na watoto, wewe unakula raha huku. Tena usivyo na haya umevaa na nguo mpya kabisa za Valentine, leo utanitambua,” dada huyo alisikika akisema kwa sauti huku akiendelea kumpa kichapo.
Jamaa (mume) alipoona soo limekuwa kubwa, alitimua mbio na kuacha timbwili likiendelea.
AZIMIA
Kipigo kilikuwa kikali na kwa bahati mbaya watu walichelewa kuamulia ugomvi huo hali iliyosababisha mrembo aliyekuwa akichezea kichapo kupoteza fahamu.
Wasamaria wema walipoona hali imekuwa mbaya kiasi kile, waliwaamulia, kisha wakatoa taarifa kwa uongozi wa ukumbi ambapo viongozi walifika haraka na kuwakamata mwanamke aliyekuwa akitoa kichapo na wapambe wake.
WAFUMANIAJI MIKONONI MWA POLISI
Wakati walioanzisha vurumai lile wakiwa chini ya ulinzi huku mrembo yule akipepewa, baunsa mmoja wa ukumbi huo alitoka nje na kuwaita polisi ambao baada ya muda mfupi waliingia ukumbini humo.
Polisi hawakutaka kupoteza muda, waliwakamata wanawake hao kisha wakawatia pingu na kwenda nao kituoni.
Njiani, dada yule aliyekuwa amezimia alikuwa akiendelea kukupewa ili aweze kupata hewa na kuzinduka, jambo ambalo halikuzaa matunda.
Habari zilipopatikana baadaye zilieleza kuwa, wanawake wale walitiwa ndani baada ya kuchukuliwa maelezo yao wakati mrembo aliyechezea kichapo akipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kitabibu, Temeke, Dar kwa matibabu.
Zoezi hilo lilifanyika baada ya taarifa za mrembo huyo kuingizwa kwenye fomu ya polisi nambari tatu ‘(PF3), huku waliompa kichapo wakisubiri mrembo huyo apone ndipo shauri lao liendelee.
Hata hivyo, mrembo huyo alirejewa na fahamu muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini ambapo matibabu yalianza mara moja.

Socials