1. Kazi zenye mahitaji maalum :
Hizi ni kazi za fani mbalimbali ambazo serikali za nchi kadhaa hutangaza kuwa nchi husika inahitaji sana watu wa fani husika. Serikali ya nchi husika hutoa muongozo wa jinsi mashirika/asasi mbalimbali zinavyoweza wasilisha maombi ya mahitaji maalum ya kuajiri.Mfano nchi kama Afrika Kusini mwaka 2011 ilitoa muongozo ufuatao. Bofya hapa kusoma.
La msingi kukumbuka hapa ni kuwa uhitaji maalum huu sio kwamba serikali ndio inahitaji kuajiri watu hapana, ni taifa kwa ujumla- serikali, mashirika na makampuni mbalimbali ya nchi husika yanahitaji kuajiri watu wa hizo fani zenye mahitaji maalum. Kwa msingi huu,michakato na taratibu za uhamiaji –kutoa vibali vya kazi, huwa si ngumu sana kama ilivyo katika aina nyingine za kazi.
2. Kazi zenye ushindani:
Hizi ni kazi ambazo si lazima ziwe zimetangazwa kuwa za mahitaji maalum kwa taifa, hata hivyo mashirika na makampuni ya nchi husika hushindana katika kupata watu bora wa kufanya kazi husika. Mfano wa kazi hizo ni graphics designers,
3. Kazi za kawaida: Hizi ni aina nyingine ya kazi ambazo haziingii katika makundi yaliyotajwa hapo juu. Mfano kazi za mikataba ya muda mfupi, kubadilishana wafanyakazi –mfano mtanzania kuhamia Kenya na Mkenya kuhamishiwa Tanzania. Kundi hili pia linajumuisha ajira kwa wanamichezo na wasanii.
Jinsi ya kupata taarifa za ajira za nje ya Tanzania
Unaweza kupata taarifa za nafasi za kazi zilizopo huko nje ya Tanzania kwa kupitia njia mbalimbali kama vile:-
1.Marafiki/Ndugu na jamaa waishio nje ya Tanzania:
Kwa kutumia marafiki , ndugu , na jamaa ambao wana taarifa sahihi na zinazoweza kukusaidia kuhusu soko la ajira, unaweza kujikuta unapata taarifa muhimu. Nafasi nyingi zinaweza kuwa zinapatikana ila hazitangazwi kwenye vyombo vya habari , hivyo marafiki, ndugu , na jamaa waishio huko nje ya Tanzania, wanaweza kukudokeza ‘michongo’ iliyopo na jinsi unavyoweza kuifanyia kazi. Ni muhimu kudadisi vema ili ujue aina ya kazi, sifa zinazohitajika , malipo na mazingira ya kazi kabla haujafanya maamuzi ya kusafiri kwenda kuapply au kufanya interview.
2.. Mitandao ya kijamii:
Ukitembelea baadhi ya pages za mashirika na makampuni hutangaza nafasi za kazi kwa kurasa zao za mitandao ya kijamii. Mfano mzuri ni Microsoft Africa kama unavyoweza jionea tangazo hili hapa chini kwenye picha, toka kurasa yao ya Facebook:
3. Website za Makampuni na Mashirika:
Tembelea websites na hata blogs za mashirika na makampuni mbalimbali yaliyopo nje ya Tanzania, na tazama kama wameweka tangazo/matangazo ya nafasi za kazi.
4. Website za mawakala wa ajira (Recruitment Agents):
Kuna mashirika au makampuni maalum yanayojishughulika na kuajiri kimataifa. Mawakala hawa hutangaza nafasi za ajira na pia hutoa maelezo ya mchakato wanaotumia kufanikisha mtu kupata ajira. Hata hivyo kuwa makini na mawakala hewa wanaotanguliza kudai malipo. Baadhi ya Mawakala wa ajira na websites zao ni kama ifuatavyo:
5.Websites za watangazaji wa ajira:
Kuna websites kadhaa zenye kujishughulisha na kuweka hewani matangazo ya ajira kutoka mashirika, makampuni mbalimbali na mawakala wa ajira. Unaweza ku search kwa kutumia Google kwa kuandika neno mfano Accounting jobs in Sudan, na kupata maelezo majibu ya Google yakiorodhesha websites za watangazaji wa ajira au websites za mashirika/makampuni husika. Pia waweza tembelea websites za watangazaji wa ajira maarufu kama vile:
6. Linkedin:
Mtandao maalum kwa watu wa fani mbalimbali, ambapo pia makampuni na mashirika mbalimbali hutangaza nafasi za ajira. Pia waweza chagua huduma ya Linkedin ambapo utakuwa ukitumiwa taarifa za nafasi za kazi kwa kadri ya uzoefu na ujuzi wako uliorodhesha katika wasifu wako, na pengine kwa uchaguzi wa aina ya nafasi za ajira unazotaka kufahamu. Usisubiri mpaka utumiwe matangazo, waweza tembelea kurasa husika za mashirika na makampuni humo Linkedin na kutambua nafasi za ajira zinazotangazwa.
Taarifa kutoka kampuni au shirika ulilopo sasa: Pengine kampuni au shirika ulilopo lina utaratibu wa kubadilisha maeneo ya kazi ya wafanyakazi wake. Fuatilia kujua mchakato mzima wa kubadilishwa eneo la kazi upoje, masharti na lini mabadiliko (transfer) hayo hufanyika. Hii inaweza kuwa nafasi yako ya kujiandaa kuhamishiwa nje ya Tanzania kwani waweza kutambua vigezo ya kiutendaji au kielimu unavyotakiwa kuwa navyo ili upewe ‘promotion’ ya kuenda nje ya Tanzania.
Masharti ya kufanyakazi nje ya Tanzania
1. Uhakiki wa vyeti vyako:
Baadhi ya nchi za nje hutaka kuwa waombaji wote wa vibali vya kazi wahakiki vyeti vyao kupitia mamlaka au taasisi maalum ya nchi hizo ili kujiridhisha kuwa kweli vyeti vyako ni halali, na kwamba aina ya kiwango cha elimu ulichonacho kinaendana na viwango vya elimu vya nchi hizo.
2. Kuandikishwa katika mamlaka au wakala fulani wa fani husika:
Baadhi ya nchi za nje hutaka kuwa waombaji wote wa vibali vya kazi wawe wamehakikiwa na kuandikishwa na mamlaka zinazohusika na fani ambayo muombaji wa kibali cha kazi anataka . Mfano kama ni mhasibu basi awe ameandikishwa na bodi ya wahasibu ya nchi husika.
3. Kuwa na Passport:
Ni lazima uwe na passport halali na pia isiwe imeisha muda wake, na kwamba wakati wa kuomba kibali cha kazi , ni lazima uwe na viza isiyoisha,yaani bado una uhalali wa kuishi nchi husika walau kwa mwezi mmoja zaidi kama unafanya maombi ya kibali cha kazi ukiwa katika nchi husika huko ughaibuni.
4. Malipo ya kibali cha kazi:
Malipo ya kibali cha kazi, hutofautiana kati ya nchi na nchi.
5.Taarifa ya polisi:
Hii ni taarifa ambayo polisi nchini Tanzania wataitoa kueleza kuwa wewe si mhalifu au mhalifu. Kabla ya polisi kutoa taarifa hii hufanya uchunguzi wa maabara wa alama zako za vidole.
Mambo Mengine ya msingi kuzingatia
1. Lugha:
Lugha ndio kiungo cha mawasiliano, kwahiyo ni muhimu kutambua lugha kuu ya mawasiliano ya eneo husika, na kujitahidi kuweza kuzungumza kwa ufasaha na pia ujiandae kujifunza lugha ndogo za mawasiliano ya kila siku. Mfano mzuri wengi hujidanganya na ‘Kiswanglish’ yaani kule kuzungumza kiswahili kisha ukachomekea na maneno machache ya kiingereza basi ndio ukajiona unaifahamu lugha. Jitahidi uiweze vema lugha husika kwani huko uendako hautopata muda wa kuchanganya kiswahili na lugha ya kigeni. Hata hivyo ni jambo la kukumbuka ukiwa makini na kwa jitihada za uhakika, utaweza kujikuta unaifahamu vema lugha ngeni kwa haraka.
2.Utofauti wa tamaduni:
Kuna tofauti nyingi za jinsi watu wanavyoishi katika nchi nyingine , mfano aina ya vyakula wanavyokula, mavazi, jinsi wanavyoheshimiana, kusalimiana, kuabudu, aina za nyumba, usafiri, n.k Uwe tayari kukabiliana na utofauti huo wa tamaduni na ujifunze kuheshimu tamaduni za wengine.
3. Gharama za maisha:
Inapendeza zaidi ukifanya utafiti wa gharama za maisha za nchi husika unayotarajia kuishi ili kujua jinsi kipato chako kitakavyotumika na jinsi utakavyoweza kuweka akiba kwa ajili ya shughuli nyinginezo za ndoto zako. Nchi nyingi zilizoendelea zina gharama kubwa za maisha hivyo kujikuta unaishia kutumia sehemu kubwa ya mapato yako kwa kula na kujikimu tuu.
4. Ajira ni bidhaa:
Mtu,shirika au kampuni, hutangaza nafasi ya kazi ili kuweza kupata mtu atakayefanyika shughuli fulani kwao. Hivyo kuendana na ujuzi wako na uzoefu wako, unajikuta unatakiwa uwahakikishie au uwaridhishe hao waajiri kuwa kweli utaweza kufanya hayo wanayotaraji wewe kufanya. Hii ni kama kuuza bidhaa, ambapo ni lazima kumfanya mteja aone sababu ya kununua bidhaa yako. Andaa vema wasifu wako (CV/RESUME), andika kwa ufasaha barua ya maombi ya kazi ukijieleza vema kwa kulinganisha maelezo ya nafasi husika unayoomba, uzoefu wako na ujuzi wako. Usikate tamaa pale maombi yanapokosa majibu, endelea kuaply sehemu nyingine.
5. Utayari wa kuishi katika nchi husika:
Inapendeza pia ukapata taarifa za awali kuhusu nchi husika unayofikiria kufanya kazi. Tumia mitandao ya kijamii, websites na hata mawasiliano ya moja kwa moja ya watu waishio huko ili kujua hali ya hewa, tamaduni, gharama za maisha na mambo mengine unayoona yanaweza kuathiri maisha yako. Pia ukiwa na nafasi wewe mwenyewe funga safari uende kuitembelea nchi husika ukae walau mwezi mmoja au wiki kadhaa hivi, ili kujifunza zaidi kuhusu nchi husika na kujipima kama kweli upo tayari kuishi nchi husika.
N:B: Maelezo haya si ushauri binafsi kwako msomaji kuhusu kupata ajira. Lengo ni kutoa tuu mtazamo wa mwandishi wetu kuhusu soko la ajira nje ya Tanzania.