Karatu. Wakati Kamati Kuu ya Chadema ikijipanga kuwahoji Zitto Kabwe na wenzake waliosimamishwa, Mwenyekiti wa chama hicho katika Kanda ya Kaskazini, Mchungaji Israel Natse, amesema salama ya chama hicho ni kuwatimua wote waliovuliwa nyadhifa zao.
Kamati Kuu ya Chadema, imepanga Ijumaa na Jumamosi wiki hii, kusikiliza utetezi wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo ambao wamevuliwa nyadhifa zao kwa madai ya kukihujumu chama.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye Viwanja vya Rotya, wilayani Karatu, baada ya kuwapokea zaidi ya viongozi na wanachama 50 wa CCM waliojiunga na chama hicho, Mchungaji Natse alisema, dhambi ya usaliti aliyokuwa akiitenda Zitto na wenzake, hukumu yao ni kufukuzwa kwenye chama.
“Mimi nitaondoka Karatu, kesho kwenda jijini Dar es Salaam kuhudhuria kikao cha Kamati Kuu, naomba msubiri uamuzi na mjue Chadema kamwe haitakufa kwa kufukuza kiongozi yeyote,” alisema Natse.
Natse ambaye pia ni Mbunge wa Karatu alisema hakuna namna rahisi ya kupata amani ndani ya Chadema kwa sasa zaidi ya kuwafukuza wasaliti.
Alisema chama hakiwezi kumvumilia mtu mmoja anayefanya jitihada za kukivuruga.
Mwigamba amshangaa
Hata hivyo akizungumza na gazeti hili jana, Mwigamba alisema: “Kwanza huyo Natse si mjumbe halali ya Kamati Kuu, yeye ni Mwenyekiti wa Kanda, cheo ambacho hakipo kikatiba na amekuwa akialikwa tu kwenye vikao. Hana hata ruhusa ya kupiga kura au kutoa uamuzi lakini cha ajabu mara kwa mara amekuwa mmoja wa wazungumzaji kwenye vikao vya kamati kuu jambo ambalo ni batili.”
Mwigamba ambaye alikiri kuitwa kujitetea Ijumaa na Jumamosi, alielezea kushangazwa kuona kile alichokiita kuwa ni kiini macho wakati tayari uamuzi umeshafanyika nje ya vikao halali na kwamba kinachofuatia ni hitimisho tu.
Natse aeleza madhambi yao
Akizungumzia baadhi ya makosa ya viongozi hao, alisema, Zitto, Mwigamba na Dk Kitila Mkumbo walikuwa wakipanga usaliti ili kukivuruga chama hicho jambo ambalo kamwe halivumiliki.
Alisema wakati wakiwa katika mkutano wa Baraza la Uongozi mkoani Arusha, walikamata kompyuta mpakato ya Mwigamba na kukuta andiko la njama za viongozi hao kukisambaratisha chama hicho, kutokana na kuandaa safu za uongozi kuanzia ngazi ya taifa hadi wilaya kinyume na utaratibu.