Dar/Iringa. Serikali imesema itaweka wazi kilichomuua Dk William Mgimwa Jumapili, huku Katibu wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, Martini Simangwa akisema marehemu Mgimwa atazikwa Jumatatu katika Kijiji cha Magunga kilichopo Kata ya Maboga mkoani Iringa.
Mwili wa Dk Mgimwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, unatarajiwa kuletwa nchini kesho ukitokea Pretoria, Afrika Kusini. Mgimwa alifariki dunia katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic iliyoko Pretoria alikokwenda kwa matibabu.
Wakati hayo yakielezwa, Serikali imeahidi kuweka wazi kilichomuua Dk Mgimwa wakati wa kumuaga marehemu Jumapili kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge,William Lukuvi, alisema kuwa kwa sasa ni mapema kueleza kilichomuua Dk Mgimwa.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Msemaji wa familia, Charles Nyato alisema mwili utawasili saa 7.00 mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) na kupelekwa nyumbani kwake Mikocheni B, Mtaa wa Ruvu.
“Baada ya shughuli ya kuaga, siku hiyohiyo, mwili utasafirishwa kwa ndege kwenda kijijini, Magunga ukipitia Iringa mjini kutoa nafasi kwa wananchi kutoa heshima za mwisho kisha kwenda kijijini ambako mwili utalala kabla ya mazishi Jumatatu,” alisema Nyato.
Dk Shein atuma salamu
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za rambirambi Rais Jakaya Kikwete kutokana na kifo cha Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.
Katika salamu hizo, Dk Shein amemwelezea marehemu kwamba atakumbukwa kutokana na utumishi wake uliotukuka kwa Serikali na wananchi wa Tanzania.
“Tanzania imempoteza kiongozi shupavu, mpenda kazi, mzalendo na mtu mwenye busara na upendo kwa wenzake,” alisema.
Naye mtoto wa marehemu, Godfrey Mgimwa akizungumzia kifo cha baba yake alisema: “Kifo cha mzee ni pigo kubwa sana kwetu, inauma ila ndiyo mipango ya Mungu.
“Mzee alikuwa ni mtu anayependa haki na mpenda maendeleo, kiongozi bora na alikuwa akifanya kazi vizuri serikalini. Tumempoteza mtu muhimu sana,” alisema Godfrey kwa upole.