JESHI LA NIGERIA YABAINI WALIKOFICHWA WASICHANA 200 WALIOTEKWA NA BOKO HARAM LAKINI HAWAWEZI KUTUMIA NGUVU KATIKA KUWAKOMBOA.
Jeshi Nigeria: twajua waliko wasichana.
Jeshi nchini Nigeria linasema kuwa linajua wanakozuiliwa zaidi ya wasichana 200 waliotekwa nyara majuma sita yaliyopita lakini likasema haliwezi kutumia nguvu kuwakomboa. Afisa wa cheo cha juu jeshini - Mkuu wa Jeshi Alex Badeh - aliwaambia waandamanaji jijini Abuja kuwa hangeweza kufichua waliko wasichana hao lakini akaahidi kuwa wanajeshi watawarejesha nyumbani wasichana hao.
"Habari nzuri kwa wasichana ni kuwa tunafahamu waliko lakini hatuwezi kuwambia. Hatuwezi kuja na kuwambia siri za kijeshi hapa," mkuu wa wanahewa Alex Badeh aliwambia waandamanaji jijini Abuja.
Alisema anaamini kuwa watawarudisha wasichana hao nyumbani hivi karibuni lakini akaeleza masikitiko yake kwa kile alichosema watu kutoka nje ya nchi wanaochochea ghasia na maandamano.
Bwana Badeh alisisitiza kuw kutumia nguvu kujaribu kuwakomboa wasichana hao ni hatari.
"Wapiganaji hawa wanataka kupigana na kwa hivyo wasichana watakuwa hatarini ikiwa kutatokea mkabiliano makali kati ya wapiganaji hao na jeshi la Nigeria," Alex Badeh alisema.BBC