MATAPELI VYUONI WAZIDI KUJA NA MBINU MPYA
Nimeona leo nilete habari hii kwasababu naamini itaweza kuwasaidia wadau wengi sana.
Kwa sasa nchini kwetu Tanzania ukosefu wa ajira unazidi kuchukua kasi na sio tu kwa ambao wanaonekana hawana elimu bali hata wale wenye vyeti mbalimbali vya chuo kwa ngazi mbalimbali kama cheti,astashahada na shahada.
Kwa sasa Tanzania ina idadi ya watu zaidi ya milioni 45,kwamaana hiyo idadi ya ongezeko la watu kila siku yazidi kuongezeka tofauti na miaka ya zamani.
Ongezeko hili la watu linafanya watu wengi sana kuona fursa za kuwa na maisha mazuri zipo mijini tu na kuondoka sehemu zao hususani vijijini wakiamini wakiwa huko hawatapata fursa za mafanikio ambacho hicho kitu kwangu mimi naona hakipo sahihi na naamini popote pale fursa zinaweza kupatikana na sio mijini tu.
Kutokana na ukosefu mkubwa wa ajira, kuna wengine wameamua kujipatia pesa kwa njia ambazo sio za halali yaani kuwadanganya watu kuhusu mambo flaniflani ambao hao ndio wanaoitwa MATAPELI.
Naomba nitoe mfano ambao umenitokea mimi mwenyewe hivi karibuni:
Mimi nilibahatika kumaliza shahada ya ualimu na sanaa (bachelor of education arts) katika chuo kikuu cha Tumaini tawi la Iringa mwaka jana 2013.Taaluma niliyosomea huwa tunapangiwa ajira na serikali (posts),lakini huwa napenda sana kuwa Tutorial Assistant (Kufundisha chuoni), kwahiyo nikaona ni bora nitume maombi kwenye vyuo ili nifanye ninachokipenda zaidi.
Niliweza kutuma maombi katika vyuo mbalimbali hapa nchi kwetu huku nikiendelea kusubiri majibu.
Hivi karibuni nilipigiwa simu na waliojiita wafanyakazi wa chuo kimoja cha serikali kilichopo pale Kigamboni hapa Dar es Salaam, ambapo ilikuwa jumamosi ya wiki iliyopita kwamba wameona CV yangu na wakawa wanaisoma mbele yangu kupitia simu.Mtu wa kwanza aliniambia kuwa yeye anatoka kwenye idara ya Data Base na akaniambia nimpigie kiongozi wake ili anipe ratiba zote za interview.
Nilipompigia huyo mtu wa pili alinieleza kuwa nina vigezo vyote vya kufanya kazi nao na aliniambia nije alhamisi yaani leo tarehe 13/3/2014 nikiwa na passport size 4,ila wao kama chuo huwa wana utaratibu wao kwa wafanyakazi wapya yaani unatakiwa kulipia gharama ya elfu 35,800 kwaajili ya usajili wa mambo mbalimbali ya hapo chuoni.Na fedha hizo natakiwa nije nazo siku hiyo ya interview.
Pesa hiyo ilinishtua mara ya kwanza na kumuhoji kuwa inakuwaje interview unatakiwa kulipia????
Alichonijibu ni kuwa hulipii interview na hamna sehemu yoyote ya malipo hayo ila hiyo pesa ni kwaajili ya usajili wa mambo kadhaa ya hapo chuoni.
Mimi binafsi nilianza kutilia mashaka juu ya kazi hiyo na kuamua kufanya uchunguzi wangu kabla ya siku hiyo kufika.
Uchunguzi niliufanya kwakushirikiana na baba yangu.Yeye alikwenda pale chuoni na kuanza kuhoji kwanza kuhusu uwepo wa hao wafanyakazi wawili.
Niliamua kumuomba mzee aende ili iwe rahisi kuwagundua ili kama hautakuwa udanganyifu basi wasiweze kunitilia mashaka siku hiyo ya interview.
Mzee wangu alipofika pale aliweza kuingia idara mbalimbali na kuhoji pasipo kunitaja jina juu ya utaratibu woote wa wafanyakazi wapya na uwepo wa hao wafanyakazi.Lakini idara zote alizoingia walimwambia kama chuo cha serikali hakina utaratibu huo na mara nyingi utumishi ndio wanaleta watu ingawa hata chuo kina nafasi yake.
Na katika interview lazima kuwepo na afisa wa utumishi pamoja na watendaji wengine wa hapo chuoni.Vilevile hakuna malipo yoyote mtu atatakiwa kulipia kwaajili ya interview.
Mwisho walimaliza na kusema kuwa hao ni matapeli tena wanatakiwa wakamatwe.
Baada ya majibu hayo nilijaribu kuwatafuta wale wahusika siku ya jana na leo ili niwasikilize zaidi watasemaje,kiukweli mpaka sasa kila nikimbana kwa maswali yule mkubwa wao anajifanya yupo bize sana na akisema atanipigia yupo bize kidogo,na amefanya hivyo zaidi ya mara 4.
Na mapaka sasa hawajanitafuta tena.
Hapo ndipo nilidhibitisha kuwa hawa ni matapeli wanaotumia fursa ya watu wanaotafuta kazi hususani vyuoni kuwalaghai.
Nitoe angalizo kwa yeyote anayetafuta kazi,anatakiwa awe makini sana na interview.Ukiambiwa unatakiwa kulipa gharama flani ili upate kazi ujue hapo huenda kukawa na utapeli, kwahiyo unatakiwa ufanye uchunguzi mkubwa binafsi kabla ya siku hiyo.