ALIYEUA BAADA YA KUMFUMANIA MKEWE AKIFANYA MAPENZI KICHAKANI,AHUKUMIWA JELA MWAKA 1,KWA KUUA BILA KUKUSUDIA HUKO TABORA
Kijana Sanane Machimi akiwa mahakama ya hakimu mkazi mfawidhi mkoa wa Tabora muda mfupi baada ya kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja kufuatia kosa la mauaji ya bila kukusudia. |
Mahakama ya hakimu mkazi mfawidhi mkoa wa Tabora imemuhukumu kutumikia kifungo cha mwaka mmoja Jela kijana anayefahamika kwa jina la Sanane Machimi baada ya kupatikana na hatia ya kuua bila kukusudia.
Akisoma maelezo ya kosa mbele ya mahakama hiyo,Mwanasheria upande wa Jamhuri Bw.Nestory Paschal aliieleza mahakama hiyo kuwa mshtakiwa Sanane Machimi akiwa na umri wa miaka 17 mnamo tarehe 7 mwezi wa 5 mwaka 2012 alimuua bila kukusudia mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Kweji Ntuvilo kwa kumpiga kwa fimbo kichwani na ubavuni baada ya kumfumania anafanya mapenzi na mkewe eneo la vichakani huko wilayani Sikonge.
Mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 195 kanuni ya adhabu sura namba 16 marejeo ya sheria ya mwaka 2002 ambapo alieleza kuwa baada ya kumkuta marehemu akifanya tendo la zinaa na mkewe haikuwa rahisi kwake kuvumilia kitendo hicho na hivyo kushikwa na ghadhabu ya kumshambulia hali iliyosababisha kifo cha marehemu Kweji Ntuvilo aliyekuwa na umri wa miaka 30.
Akisoma hukumu baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, hakimu mkazi mwandamizi mwenye mamlaka ya ziada Bw.Thomas Simba alisema mahakama hiyo tukufu imepitia kwa makini shitaka hilo na kumtia hatiani Sanane Machimi ambapo alimhukumu kutumikia kifungo cha kwenda Jela kwa muda wa mwaka mmoja ili iwe fundisho kwa mtu mwingine atakayediriki kufanya kosa kama hilo.
Hata hivyo mshtakiwa mara baada ya kusomewa adhabu hiyo alisikika akimshukuru Mwenyezimungu akidai kuwa adhabu aliyoipata imekuwa na nafuu sana kwake kwakuwa tayari alikuwa amekaa mahabusu tangu mnamo mwaka 2012.