Stori: Haruni Sanchawa na Denis Mtima
SIMU ya Kichina imezua balaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Jumatano iliyopita wakati wa usikilizwaji wa kesi ya Katibu wa Jumuiya ya Kiislamu, Shehe Ponda Issa Ponda, Ijumaa linakupa habari kamili.
Baadhi ya wafuasi wa Shehe Ponda, wakijadiliana jambo (katikati) ni Shehe Kitula ambaye simu yake ilizua balaa.
Tukio hilo la aina yake lilitokea baada ya simu ya Kichina ya mmoja wa wafuasi wa Shehe Ponda aliyefahamika kwa jina la Shehe Kitula kuita wakati shughuli za kimahakama zilizopokuwa zikiendelea.
Wakati jaji wa mahakama hiyo, Augustino Mwalija akitahamaki kwa kitendo hicho, askari waliokuwepo mahakamani hapo walimkamata Shehe Kitula anayeswali katika Msikiti wa Masjidi Haki uliopo Buguruni jijini Dar na kwenda kumhoji.
Wafuasi wa Shehe Ponda wakiwa na shehe Kitula.
Baadhi ya waumini walipinga kitendo cha Shehe Kitula kukamatwa na kutaka kufanya fujo ili asiingizwe kwenye chumba cha mahojiano lakini walitulizwa na wenzao.
Shehe Kitula alipohojiwa na waandishi wetu alikiri kuchanganywa na simu hiyo baada ya kusahau kuizima alipoingia mahakamani hapo.
Wafuasi wa Shehe Ponda wakipanga mikakati nje ya mahakama.
“Nilisahau kuizima simu, polisi walikuwa na haki ya kunikamata kwa kuwa sheria hairuhusu kelele mahakamani,” alisema shehe huyo.
Kesi ya msingi, Shehe Ponda anashtakiwa na serikali kwa kosa la kutoa lugha za uchochezi alipokuwa akihutubia moja ya mikutano yake ya hadhara mjini Morogoro mwaka jana.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 26, mwaka huu ambapo mwanasheria wa serikali atatakiwa kujibu hoja za mwanasheria wa Shehe Ponda, Juma Nassoro.
Wakati huo huo, Jaji Mwalija anaweza kumpa dhamana Shehe Ponda au kumnyima.