Stori: Jelard Lucas
ULE uvumi kwamba baadhi ya wachungaji na maaskofu wa makanisa ya kiroho nchini wanajihusisha na imani ya Freemason unazidi kushika kasi huku awamu hii ‘rungu’ likimwangukia Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo jijini Dar, Lusekelo Antony ‘Mzee wa Upako’ na kutikisika, Uwazi lina cha kusema.
MINONG’ONO ILIVYOANZA
Madai ya mtumishi huyo kujihusisha na imani ya Freemason yalianza kuenea kwa kasi mithili ya moto nyikani huku baadhi ya watu, wakiwemo watumishi wa makanisa ya Kikristo, wakionesha shaka juu ya uponyaji wa mtumishi huyo kufuatia miujiza ya ajabu ambayo amekuwa akiionesha kwa watu wenye uhitaji wa kiimani.
MATENDO YA SHAKA
Baadhi ya matendo ambayo yamekuwa yakiwatia shaka baadhi ya watu ni pamoja na kitendo cha mchungaji huyo kuwaombea watu wakiwa hawana kitu kabisa lakini baada ya miezi michache hurudi kanisani hapo wakiwa na magari ya kifahari na wakionesha kila dalili ya ukwasi (utajiri).
“Eti unakuta mtu amekwenda kuombewa akiwa hana kitu kabisa (fukara) lakini bada ya miezi michache anarudi akiwa na gari la kifahari, kweli?
“Tena anaonesha kila dalili ya ukwasi, huenda ni kweli kuna nguvu za ziada zaidi ya ile ya kiroho,” walisema baadhi ya waumini wa makanisa mbalimbali ya Kikristo walipozungumza na gazeti hili hivi karibuni.
ALAMA NA VIASHIRIA TATA
Wakifafanua kwa kina zaidi juu ya wasiwasi wao kwa Mzee wa Upako na miujiza yake, waumini hao walitolea mfano wa baadhi ya dalili na viashiria tata vinavyoshukiwa kuwa ni moja ya utambulisho wa Taasisi ya Freemason.
Wakitaja baadhi ya alama hizo, waumini hao walisema mara nyingi mtumishi huyo akiwa madhabahuni amekuwa akitumia kitambaa kikubwa.
“Kila akiwa jukwaani au madhabahuni hutumia kitambaa kikubwa kujifutia na kuwagusia anaowaombea hali ambayo huwafanya kuanguka na kupiga kelele hovyo,” walisema.
Mbali na kitambaa, pia walisema Mzee wa Upako amekuwa akionekana na pete zenye picha za ajabu akiwa anahubiri au kutenda miujiza.
MADAI ZAIDI
Baadhi ya waumini hao walisema viashiria vingine ni kitendo cha mchungaji huyo kutotaja neno Mbinguni katika mahubiri yake zaidi ya kusema, ‘Mungu wangu awabariki sana’.
“Mapete yake yana mapicha ya ajabu sana, yale maalama ya Freemason yapo, pia huwa hawezi kusema Mungu wa Mbinguni, badala yake husema ‘Mungu wangu awatangulie’ au ‘kwa uwezo wa Mungu ninaye mwabudu’ jambo ambalo hututia shaka sana,” walisema Wakristo hao.
WAUMINI WAMBANA
Katika kufuatilia kwa kina sakata hilo, habari zikadai kuwa baada ya mambo kupamba moto waumini wa kanisa lake walianza kumbana mtumishi wao huyo kuhusu uvumi huo huku baadhi yao wakianza kutimkia kwingine.
“Ni kweli zahama hiyo iliwahi kutokea, lakini mambo yalikaa sawa baada ya baba (Lusekelo) kutufafanulia zaidi juu ya madai hayo,” alisema mmoja wa waumini wa kanisa hilo kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini.
LUSEKELO KIZIMBANI
Baada ya ‘viranja’ wetu kupata taarifa hizo nzito, hivi karibuni waliamua ‘kukanyaga lami’ hadi kanisani kwa mchungaji huyo, Ubungo -Kibangu ambapo licha ya kukumbana na vikwazo mbalimbali walibahatika kukutana naye na kumbana kwa maswali juu ya tuhuma hizo ambapo kwa ‘jasho jembamba’ aliweza kueleza kwa kina:
“Hizo tuhuma zilianza kusikika zamani sana, watu walianza kunituhumu kwenye matumizi ya bendera ya taifa kanisani, nikatoa, wakahamia kwenye kitambaa.
“Jamani natumia muda mwingi sana kusimama madhabahuni. Sasa nikitumia kitambaa (hendkachifu) cha shilingi mia tano itawezekana kweli, natumia kitaulo kidogo kujifutia jasho, sasa inaonekana nongwa.
“Baadaye wakahamia kwenye pete! Mimi ni mtu smart sana (msafi) nimezaliwa mjini (born town) sasa kuvaa pete ni sehemu ya maisha ya mjini sioni tabu, lakini baada ya manenomaneno nilivua na sasa sina,” alisema Mzee wa Upako.
KUHUSU WAUMINI KUTIMKA
“Ni kweli, baadhi waliniuliza nikawajibu, wengine wakaamua kutimka. Unajua mimi nimeanza kumtumikia Mungu kwa miaka thelathini sasa, muumini kuhama kanisa na kwenda kwingine sishangai.
“Lakini wajue kwamba hapa kwangu ni moto mkubwa, super charge, cartapillar, siteteleki, nitazidi kuwaombea na kuwaponya wenye taabu na magonjwa,” aliongeza.
KUHUSU FREEMASON?
“Sijawahi kufikiria hata siku moja kuwa Freemason, kwanza sifahamu hata wanavyopatikana, nimeanza kumtumikia Mungu nikiwa kijana mdogo, mimi si muumini wa dini wala imani yoyote ya kishetani.
“Shetani mwenyewe ananiogopa, sasa hao wanaosema kuwa huwa sisemi Mungu wa Mbinguni, nashangaa, ni lazima kuweka neno Mbinguni? Jamani hao Freemason siwajui, wala siwazuii watu kuniita hivyo, naendelea kulihuburi Neno la Mungu aliye hai,” alisema Lusekelo na kufunga ‘faili’ la mazungumzo na waandishi wetu.