AKAMATWA AKIDAIWA KUUZA NYAMA YA BINADAMU
Mkazi wa Kijiji cha Kihinga, Kata ya Bugarama wilayani Ngara mkoani Kagera(jina tunalo), anashikiliwa katika kituo kidogo cha polisi cha kata hiyo baada ya kutuhumiwa kuuza kilo moja ya nyama ya binadamu kwa Sh100,000.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kihinga, Hassan Mohamed alisema kuwa jana saa mbili usiku, wananchi walipeleka fedha nyumbani kwake kununua nyama hiyo na alipowaona alikimbia na wananchi hao kwa hasira walimkimbiza ili kumuua na hapo hapo kuunguza nyumba yake.
“Mgambo ndio walimnusuru asiuawe na wananchi wenye hasira kali na alikimbizwa kituo kidogo cha polisi Kata ya Bugarama ili kuokoa maisha yake “.
Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa mgambo wa kijiji hicho, Emanuel Kaloli alisema wananchi waliandamana baada ya kusikia taarifa za kuwapo mtu anayeuza nyama ya binadamu na kutaka kuhakikisha ukweli huo.
Alisema baada ya wananchi kufika, walianza kumshambulia na kutaka kumuua, lakini wanamgambo wa kitongoji walifika kisha kumuokoa mtuhumiwa na hatimaye kumfikisha kituo cha polisi kwa ajili ya usalama wake.
“Kijana aliyefahamika kwa jina la Man Balyamwabo mkazi wa Shina la Kalenge katika kitongoji hicho, ndiye aliyeambiwa kuwa angeuziwa nyama hiyo ya binadamu na kuleta taarifa katika uongozi wa kijiji ili uweze kuchukua hatua zaidia”.Alisema Kaloli.
Alisema nyumba aliyounguziwa pamoja na mali iliyokuwamo ndani hasa maharage, mavazi na vitu vinginevyo inakadiriwa kuwa na thamani ya Sh2.6milioni. Pamoja na kuwepo kwa tukio hilo, baadhi ya wananchi walisema mtuhumiwa inasemekana ni raia wa nchi jirani ya Burundi na alianza kuishi katika kitongoji hicho tangu mwaka 1981 kama kibarua wa kilimo kwenye mashamba.
Taarifa zinasema kuwa katika kuishi kwake na ndugu yake aliyefahamika kwa jina la Kahungu walikuwa wakituhumiana kwa uchawi na ilifikia mahala wakatofautiana na kaka yake ambaye alirejea kwao.
Polisi wilayani Ngara imethibitisha kumpokea mtuhumiwa huyo na kwamba linafanya mahojiano ya kina kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji ili kubaini ukweli wa tukio hilo.