ARIEL SHARON AFARIKI DUNIA

Israel. Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel, Ariel Sharon (85) amefariki dunia Hospitali ya Sheba Medical Centre alipokuwa akipatiwa matibabu ya afya ya viungo hususan figo kwa kipindi cha miaka minane.
Akitangaza kifo cha waziri mkuu huyo kwenye mkutano na waandishi wa habari jana, Mkuu wa hospitali hiyo, Profesa Shlomo Noy alisema: “‘Leo (jana) Sharon ametutoka kwa amani na upendo akiwa na familia yake pembeni.”
Profesa Noy alisema Sharon alitibiwa kwa zaidi ya miaka saba kwenye kituo hicho na kwamba, alikuwa katika hali ambayo hairidhishi ambayo madaktari walihangaika kuhakikisha wananusuru uhai wake.
Alisema huu ni muda wa kuwashukuru wafanyakazi wote wa hospitali hiyo kwa kupigania uhai wake kipindi chote, walikuwa wavumilivu na kumjali.
Waziri wa Masuala ya Mipango wa Israel, Yuval Steinitz alisema taifa limepoteza shujaa.
“Taifa la Israeli leo limempoteza mtu mpendwa, kiongozi mkuu, shujaa na mwenye ujasiri,” alisema.
Sharon alikuwa waziri mkuu mwaka 2001, mwaka 2005 aliugua kiharusi kwa mara ya kwanza hivyo kusababisha utendaji wake kuanza kuzorota.
Hata hivyo, alitibiwa na kuruhusiwa kutoka hospitali akiendelea kuhudumiwa nyumbani.
Januari 2006 alipatwa tena kiharusi kilichosababisha kupoteza fahamu, madaktari walilazimika kumwekea mashine za kusaidia upumuaji.
Enzi za uhai wake alijulikana kama mwanasiasa hodari na mwenye nguvu kwenye siasa za nchi hiyo kwa kipindi kirefu.
Alizaliwa mwaka 1928 eneo la Palestina wakati huo ikiwa kwenye utawala wa Uingereza.
Mwaka 1942 alijiunga na Kikosi cha Vijana cha Gadna, mwaka 1956 alipandishwa cheo cha Brigedia kwenye jeshi la nchi hiyo kwenye vita ya Suez.

Socials