SIFA HIZI NDIYO ZINAFAA KWA MWANAMKE KUMCHUNGUZA MWANAUME MWENYE MAPENZI YA DHATI SAMBAMBA NA NIA YA KUOA, KAMA ATAKOSA SIFA HIZI BASI HUYO NI TAPELI KATIKA MAPENZI.
HII ni safu ya wale walio tayari kuambiwa ukweli hata kama utawauma. Ndiyo...siku zote ukweli huwa unauma. Karibuni sana marafiki katika uwanja wetu ili tuweze kupanuana mawazo katika mambo ya uhusiano.
Nazungumzia sifa za mwanaume ambaye ana mapenzi ya kweli. Ni mada ambayo unaweza kuiona ya kawaida sana lakini ndani yake kuna mbinu madhubuti zitakazokufanya ugundue kuwa upo kwenye uhusiano wa kweli au wa longolongo!
Hakuna mwanamke anayependa kuolewa na mume halafu waachane baada ya muda mfupi, bali kila mwanamke ana kiu ya kutaka kuishi na ampendaye mpaka kifo.
Kwa misingi hiyo,ndoa ni jambo muhimu na gumu kwa wakati mwingine hasa linapokuja suala la kuchagua mwenzi wa kuishi naye maishani.
Wanawake wengi wamekuwa wakigombana na wenzi wao wa ndoa, ama ndoa zao kuvunjika kabisa kutokana na kutoelewana.
Ikitokea ukawauliza baadhi ya wanawake ambao tayari wamekwishaachana na waume zao, au wako katika migogoro mikali, watakupa sababu za msingi ambazo huenda ikawa ni manyanyaso na mateso makali katika ndoa zao kiasi wanaona ndoa ni chungu na kuamua kutoka ndani ya ndoa hizo.
Pamoja na hayo yote zipo njia mbadala ambazo wewe mwanamke unaweza kuzitumia kumpata mume mwema katika maisha yako ya ndoa, kabla ya kuingia ndani ya ndoa hiyo ambayo inaweza kuwa ndoano.
Hebu twende tukaone kwa uchache ingawa zipo njia nyingi...
ALIYE MKWELI.
Katika hili, hekima na busara nyingi huhitajika kutumika, ngao kubwa ya utambuzi juu ya mpenzi uliyenaye kuwa mume mwema linategemea sana hili. Ukweli ni silaha muhimu sana katika uhusiano.
Japo natambua kuwa, kuna wengine watajiuliza utajuaje kama huyu ni mkweli au siyo. Kitendo cha kukutamkia kuwa, anakupenda ni cha ukweli sana hasa kama atakuwa anakupenda kwa dhati.
Cha kuzingatia hapa, anayaweka vipi maisha yake yaliyotangulia, anakueleza kwa uwazi upi hasa. Inawezekana alishawahi kuwa na uhusiano na mwanamke mwingine kabla, je amekufahamisha vipi. Chunguza kila akuambialo ili kuhakikisha ukweli wake.
Baadhi ya wanaume wanafikia hatua kuongopa na hata kuazima gari na kujifanya kuwa ni lake ili akunase. Kumbuka wahenga walisema ‘njia ya muongo ni fupi’ hivyo baada ya muda utachambua pumba na nafaka.
ANAYEJALI
Wahenga waliendelea kunena, `nyota njema huonekana alfajiri’. Huo ni msemo wa zamani wa wazee wetu ambao una maana kubwa sana. Kama mwanaume huyu ambaye kwa sasa ni mchumba wako (wazazi wawe wanatambua) anakupenda, lazima atakujali, hukuwazia wewe katika maisha yake yote, hukuona kuwa wewe ni mwenye thamani kubwa katika maisha yake.
Hatakusumbua kwa kutaka ngono kabla ya muda muafaka wa kufanya hivyo. Anayejali afya yako kwanza na hatathubutu kushiriki tendo la ndoa kabla hamjapima virusi vya ukimwi, anakupeleka hospitali unapokuwa mgonjwa (haijalishi kama una wazazi au wasaidizi wengine).
ALIYE NA MSIMAMO THABITI
Huyu huonekana mapema sana, asiyetingishika wala kushawishiwa na marafiki zake, katika mambo yasiyofaa.
Hushikilia msimamo wake katika kutekeleza yale yote aliyokuahidi na aliyopanga kuyafanya kwa ajili yenu.
Mathalani, ameambiwa na watu kuwa wewe una uhusiano na mwanaume mwingine. Mwenye msimamo huchukua muda mwingi kufanya uchunguzi juu ya aliyosikia kabla hajakuuliza chochote.
Nathubutu kusema hivyo kwa sababu kuna baadhi ya wanaume wana kasumba mbaya, wanaposikia kitu kuhusu wachumba zao, au wapenzi wao, kabla ya kufanya uchunguzi humjia juu mwanamke husika na wakati mwingine hufikia hata hatua ya kumpiga.
Hii ni hulka mbaya ambayo baadhi ya wanaume wanayo, lakini jaribu kujiuliza, kama hamjaoana anadiriki kukupiga kama ngoma na akikuoa je, si atakufanya kilema?
ANAYESHAURIKA
Siku zote, amekuwa mkweli kwako, anakubainishia mali zake pamoja na biashara zake. Haoni vibaya pia kukufundisha juu ya kuendesha mali zake. Inapotokea unamshauri, hukusikiliza kwa makini na kufanyia kazi ushauri unaompa. Mwanaume huyu hutulia na kuyapima maneno yako kwa makini kabla hajayafanyia kazi.
Ni vyema mumeo ashaurike (inapobidi) ili asifanye madhara mengine katika maamuzi ya familia kwa kisingizio cha ubaba ndiyo kichwa ca familia.
ANAYEJALI NDUGU ZAKO
Waswahili wanasema `ukipenda boga, penda na ua lake’kwa wakati mmoja, msemo huu unasisitiza upendo. Kwamba kuna vipimo kadhaa vya upendo lakini moja ni kumwangalia kama ana upendo na ndugu zako.
Mwanaume huyu mara zote hukuulizia hali ya wazee wako pamoja na ndugu zako wengine. Hii ni sawa na mawingu kabla ya mvua. Kwa sababu kama atashindwa kuwajali ndugu zako japo kwa kuwajulia hali utakapoingia katika ndoa atakuruhusu ukawasabahi kweli? Hili ni kama msingi katika kumpata mume bora.
Anza sasa kutumia mbinu hizo, utampata mwanaume sahihi katika maisha yako na hutajuta. Ahsanteni sana kwa kunisoma, usikose wiki ijayo kwa mada nyingine kali.