IMENGUNDULIKA ..............ZIJUE KWANINI WANAFUNZI WANAFANYA SAAAAAAANA MAPENZI CHUONI..................


Wanafunzi na vishawishi vya kimapenzi


Katika mada ya vizuizi vya mafanikio ya kimasomo tumeona suala la mwanafunzi kujihusisha na mapenzi limechukua nafasi ya pili, hii ina maana kuwa wanafunzi wengi hupoteza mwelekeo wa kimasomo baada ya kujiingiza katika ulimwengu wa mapenzi.

Jambo baya kabisa kwa wanafunzi ambao ni wenyeji wa masuala ya kimapenzi hivi sasa hasa wanawake ni kutokukumbuka namna walivyotekwa kimapenzi na wengi kati yao wanadai kuwa haukuwa utashi wao na kwamba walilazimishwa, aidha na watu, mazingira au misisimko ya miili, jambo ambalo si la kweli kisaikolojia.

Ninachoweza kusema katika mada hii ni kwamba wanafunzi wengi hawafundishwi masuala ya mapenzi katika familia zao na hivyo kujikuta wakiingia katika mtengo wasioufahamu madhara yake.

Wazazi, walezi na waalimu wengi wanadhani usiri katika elimu ya mapenzi ni sehemu ya heshima na kwamba kumuelewesha mtoto mambo ya kimahaba ni kumfundisha uhuni, jambo ambalo si la kweli.

Lakini kisaikolojia kumnyima mtoto elimu ya uhusiano wa kimapenzi katika ulimwengu huu wa utandawazi ni kumuua katika utashi, ambao ndiyo kitu muhimu katika maisha ya binadamu. Siku zote maamuzi ndiyo kitu pekee kinachoweza kumtofautisha mwanadamu na viumbe vingine na uamuzi sahihi haufikiwi bila elimu kamili.

Wataalamu wengi hawaamini kuwa mwili unaweza kushinda utashi wa mwanadamu na ikitokea makosa katika utendaji wowote, jambo la kwanza kumulikwa lazima litokane na ufahamu. Kwa maana hiyo mwanafunzi kufanya ngono akiwa shuleni hakuwezi kupewa sababu ya No how (isiyofahamika) isipokuwa kama nguvu ilitumika kutengua utashi.

Labda baada ya kusema hayo swali linaloweza kujitokeza miongoni mwa wanafunzi wengi ni jinsi gani wanaweza kutumia utashi wao kuepuka mambo ya uhusiano wa kimapenzi wawapo shuleni?

Jibu ni rahisi nalo ni kutambua vishawishi na kuchukua tahadhari mapema kabla ya kuikuza tamaa na kujikuta wameingia kwenye kosa la kufanya mapenzi ambayo ni hatari kwa mustakabali wa masomo.

(1) –MAKUNDI

Tumeshazungumza mengi kuhusu athari za kufuata mkumbo wa makundi, lakini kwenye kipengele hiki hatari ya kuwa na makundi ya wapenda mapenzi ni kukutia vishawishini. Uzoefu unaonesha kuwa wanafunzi wengi hasa wa kike huanza mapenzi baada ya kutekwa kihisia na rafiki zao na kuna ushahidi wa baadhi ya wanafunzi kutongozwa kwa njia ya ukuwadi.

Hivyo, mwanafunzi hatakiwi kuwa na makundi ya wapenda mapenzi, ni vema akajiepusha nayo na asithubutu kamwe kusikiliza au kuchangia mada za kimahaba. Sambamba na hilo mwanafunzi hatakiwi kuwa na mazungumzo au kutumiana meseji za kimahaba na mwenzake, akijikita katika mazungumzo ya aina hii ataushawishi mwili umsumbue.

(2)-TAMAA- Tamaa ya kupata vitu vizuri nayo inatajwa kuwa imekuwa ikiharibu msimamo wa wanafunzi wengi wao wakiwa wa kike. Uchunguzi unaonesha kuwa wanafunzi wanaosoma shule za Boarding ndiyo wanaongoza katika kutekwa na vishawishi mbalimbali ikiwemo hali ya kutamani maisha ya wengine na kutaka kuishi kama wao kwa kula vyakula vizuri na kujinunulia mahitaji mengine bila kupungukiwa.

Mwanafunzi makini hatakiwi kabisa kuendekeza tamaa ya vitu na kuingia katika mashindano ya mavazi, vyakula na anasa. Umakini zaidi unahitajika hasa pale zawadi zisizokuwa na maelezo ya kina zinapotolewa. Imebaini kuwa watoto wa kike ndiyo wanaongoza kwa kupewa ofa ambazo nyingi kati ya hizo husimama kama hongo za ngono.

Inashauriwa, zawadi zozote kutoka upande wowote zenye heri lazima zielekezwe kwa wazazi, walezi au waalimu husika, vinginevyo zinaweza kutumika kama chambo na wanafunzi wengi wameingizwa mtegoni kwa zawadi.

Ni wajibu wa mwanafunzi kugomea zawadi inayokuja kwa mlango wa nyuma, kwa vile watafiti wanasema watu 9 kati ya 10 wanaosaidia husaidia ili wajisaidie ni mmoja tu anayesaidia kwa maana ya kusaidia.

(3)-MAZINGIRA MAGUMU –Mazingira magumu yametajwa sana na baadhi ya wanafuzi kuwa yanashawishi kufanya mapenzi, lakini ukweli unabaki kuwa mwanadamu kamili mwenye kutathimini utu wake hawezi kuuza utu wake kwa kukwepa adha. Mwanafunzi hana budi kupambana sana na shida za kitambo ili atafute raha ya muda mrefu.

Kujilegeza kokote kwa lengo la kujiokoa na mateso hakujawahi kuwa na matokeo mazuri kwa mtu au taifa lolote duniani zaidi ya maangamizi. Mwanafunzi lazima afahamu kuwa kukubali kuwa mtumwa wa mapenzi ya mtu hakutamuokoa bali kutamfelisha masomo na kisha kutelekezwa na pengine kuambulia magonjwa ya zinaa ukiwemo UKIMWI.

(4)-MABADILIKO YA MWILI- Ni jambo linaloshawishi, kwani mwili unapofikia wakati wa kubalehe huleta usumbufu kwa watoto na kuwafanya wawe na tamaa ya kufanya mapenzi. Lakini tamaa hizi ni rahisi mno kuzishinda, tofauti na zile zitakazokuja baada ya mtu kuanza mapenzi. Njia pekee ya kuzishinda ni kuepuka vishawishi vyote na kuwa na maamuzi sahihi kama tunavyoendelea kujifunza.

(5)-KULAGHAIWA – Laghai kubwa kabisa ambayo inachukua nafasi ya kwanza kwa sasa ni ya ahadi za uchumba. Wasichana wengi wamejikuta wakiingia katika uhusiano wa kimapenzi na wanaume waliowachukulia kama wachumba wao. Ukweli ni kwamba matapeli wengi wa kimapenzi hutumia mwanya huu kuwadanganya wanafunzi na kuwaharibia masomo yao.

Kama wewe ni mwanafunzi, usikubali kabisa mtu akuite mchumba na akiwa na sababu ya kufanya hivyo mwelekeze kwa wazazi wako lakini wewe usizungumze naye kwa kuwa umri wako bado mdogo.

(6)MALEZI YASIYO NA MAADILI- Wazazi nao wanaweza kuchangia mwanafunzi kujiingiza katika mapenzi, kuna baadhi yao hudiriki kuwatumia watoto wao kama mitaji kwa kuwauza kwa wanaume kwa lengo la kujipatia mahitaji yao. Lakini wengine hushawishi kwa matendo yao, yaani kufanya matendo ya kihuni mbele za watoto na hivyo kuwafanya waone kama mapenzi si kitu cha hatari kwa vile baba na mama wanafanya.

Ushauri kwa mwanafunzi ni kuwa makini na kukataa kila vishawishi hata kama vinatoka kwa wazazi wao. Inaaminika kwamba kila mwanadamu ana haki ya kusimamia anachokiamini hasa kinapokuwa cha kweli, la sivyo kuacha maadili kwa sababu ya mtu mwingine hakuna tofauti na kuuza utu.

(7)KUKOSA MIPAKA- Kuna wanafunzi ambao hawaheshimu mipaka ya uhusiano kati ya wanaume na wanawake. Utakuta chumba cha wavulana, wasichana wanaingia kwa uhuru hadi usiku wa manane na wakati mwingine kuwa tayari kushikana shikana hadi sehemu nyeti za miili yao.

Tabia hii haipendezi kwani inaweza kuleta hisia za kimapezi. Inashauriwa kuwa wanafunzi wa jinsia tofauti lazima wawe na mipaka ya uhusiano kwa kuheshimiana. Haifai wanafunzi wa jinsia mbili tofautia kukumbatiana hovyo na inapotokea wakawa pamoja basi wazingatie sababu za msingi za umoja wao na si vinginevyo. Hii itasaidia kuzuia hisia za kimapenzi, kwani miili imeumbwa kwa mfumo wa sumaku.

(8) KUANGALIA/ KUSOMA MAJARIDA YA NGONO- Mwanafunzi hatakiwi kuangalia au kusoma majarida ya ngono. Kama ilivyo kwenye vipengele vingine uangaliaji wa filamu za kimapenzi kwenye video na mitandao ya intaneti hushawishi mtu kufanya mapenzi. Mwanafunzi makini lazima ajiepushe na mambo haya.

Akifanya hivyo atajikuta katika vishawishi vya mwili na hatimaye atafanya mapenzi.

(9) KUJARIBU – Kujaribu kufanya jambo ni zao linalotokana na maneno ya kusikia, kama nilivyosema huko nyuma kwamba mazungumzo ya kimapenzi hushawishi mtu kufanya mapenzi, lakini kibaya zaidi ni uamuzi wa kujaribu kufanya jambo baada ya kusikia kisha kujipa moyo kwamba likifanyika litaachwa.

Mwanafunzi hatakiwi kabisa kuruhusu akili impe majibu ya kujaribu na kudhani kuwa akishafanya mara moja ataacha, wataalamu wanasema ni rahisi mno kujizuia kwa mara ya kwanza kufanya mapenzi kuliko mara ya pili. Ikiwa mwanafunzi anataka mafanikio katika maisha yake ya shule anatakiwa kuweka kando majaribio ya vitu visivyokuwa na maana. Sumu haijaribiwi kwa kuonjwa.

Lakini jambo jingine linalotaka maamuzi sahihi ni mwanafunzi kuwa makini na kauli za kushawishi zinazoelekezwa kwake kwa njia ya udhaifu au ugonjwa, mfano: “wewe hadi leo hujaanza kufanya mapenzi, wala hujisikii chohote? Basi utakuwa na kasoro au ni mgonjwa” kauli hizi zinaweza kumfanya mwanafunzi kuuweka kando msimamo wake na kuamua kupima uzima wake.

Ifahamike kuwa mwili wa mwanafunzi makini anayeua hisia kwa kuzingatia muongozo uliomo kwenye mada hii mwili wake hauwezi kuwa na msisimko wa kimapenzi na si kwa maana ya ugonjwa au kasoro, lakini nguvu ya utashi ndiyo inayoleta zao hili. Hivyo haifai kwa mwanafunzi kuingiwa na wasiwasi wowote anapoona mwili wake hausumbui kwa maana ya kusisimka sawa na maelezo kutoka kwa wenzake walioanza kufanya mapenzi.

(10) MILA NA DESTURI POTOFU – Kishawishi kingine cha mwanafunzi kufanya mapenzi kinatokana na mila na desturi potofu ambazo huwafundisha hasa watoto wa kike namna ya kufanya mapenzi na wanaume. Ni busara kwa mwanafunzi kupinga mila hii kwa kuwaambia wazazi wake kuwa yeye bado mtoto na kwamba hapendi kujiingiza katika mapenzi hivyo wazazi wanatakiwa wamsubiri hadi akue na kama kutakuwa na suala la kumfundisha basi lifanyike wakati akiwa amemaliza shule.

Kifupi haya ni mambo machache tu ambayo yanaweza kumshawishi mwanafunzi kufanya mapenzi, lakini ili mwanafunzi awe mkamilifu katika kuyatenda haya, anatakiwa kushirikiana na wazazi na walimu wake hasa anapokutana na moja kati ya vishawishi hivi.

Ni vema kwa mtoto wa kike akawa na uhusiano mzuri na mama yake kwa lengo la kumweleza na kumuuliza kinagaubaga mambo yote yahusuyo mapenzi. Hili ni jema kwa baba na mtoto wake wa kiume.
Share !


Socials