MVUA, RADI, UPEPO VYALETA MAAFA DAR ES SALAAM.
Mwananchi lilifika katika baadhi ya maeneo na kushuhudia familia zikiwa nje ya nyumba zao na wengine wakiwa wamefungia vitu vyao ndani na kuelekea maeneo mengine wakisubiri maji yakauke ili warejee katika nyumba zao.
Samani kama magodoro, makochi na vitanda vilionekana vikiwa vimetolewa nje kutokana na maji kujaa ndani ya nyumba hizo, ishara kwamba maisha hayaendi sawa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Katika eneo la Jangwani, kuanzia ulipo ukingo wa Mto Msimbazi mpaka katika sehemu ya eneo la makao makuu ya timu ya Yanga, maji yamejaa kiasi cha kuvuka magoti ya mtu mzima.
Eneo hilo limefurika na wananchi waliohojiwa wamesema kuwa, sababu kuu ni kuzibwa kwa mfereji unaopeleka maji baharini katika Barabara ya Morogoro kutokana na ujenzi unaoendelea kwenye barabara hiyo.
Ally Mgoha (95) mkazi wa Jangwani alisema endapo mfereji unaopitisha maji ungezibuliwa basi adha hii waipatayo ingepungua kwani hivi sasa hali si nzuri katika eneo hilo.
“Wananchi tumechanga pesa ili mfereji uzibuliwe lakini tulinyimwa kibali kutoka kwa ‘wakubwa’. Sisi hatuwezi kuhama hapa kwa sababu ni kwetu na tumejenga tangu kwa kipindi kirefu…watu wametumia mamilioni ya fedha kujenga nyumba zao,” alieleza Mgoha.
Mgoha anasisitiza kuwa hata waliokwenda Mabwepande wanarudi kutokana na kuchoshwa kuishi katika mahema baada ya ahadi ya Serikali kuwapa vifaa vya ujenzi kutotekelezwa.
“Mwanangu mmoja yupo kule lakini shida azipatazo ni nyingi,
Mwananchi lilifika katika Ofisi za Serikali za Mitaa ya Mtambani ‘A’ na kushuhudia ofisi hizo nazo zikiwa zimefurika maji na baadhi ya nyaraka zilizolowa zikianikwa huku juhudi za kuyatoa maji nje ya ofisi hizo zikiendelea.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Ally Hamed alisema fedha zilizochangwa na wananchi hazitoshi kukodi vifaa vya kuzibua mfereji ili kupunguza adha waipatayo wakazi wa eneo hilo.
Katika maeneo ya Chang’ombe makaburini, Mwananchi lilishuhudia baadhi ya makaburi yakiwa yamezingirwa na maji na hata mboga zinazolimwa katika eneo hilo zikiwa zimefunikwa na maji.
Baadhi ya wakulima waliokutwa eneo hilo walieleza kuwa mvua imewasababishia hasara kwa kuwa mazao yao hayawezi kustawi tena kama walivyotarajia.