"MTUME NA NABII"MWINGIRA AGOMA KUPIMA UKIMWI

Stori: Makongoro Oging’ na Richard Bukos
MTUME na Nabii wa Kanisa la Efatha, Joseph Elias Mwingira anayekabiliwa na kesi ya kuzaa na mke wa mtu, hatimaye amefunguka mengi kuhusu madai hayo lakini amekataa kabisa kupima Ukimwi, Risasi Mchanganyiko lina kila kitu.
Mtume na Nabii wa Kanisa la Efatha, Joseph Elias Mwingira.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi - Kisutu, Dar, umebaini kuwa Mwingira aliye na kesi mahakamani hapo yenye namba 306 ya 2013, iliyofunguliwa na mlalamikaji Dk. Morris William, amejibu tuhuma zinazomkabili kwa njia ya maandishi.
Majibu hayo yameandaliwa na Kampuni ya Uwakili ya Legal Link, ambapo nakala yake imefikishwa kwa wakili wa mlalamikaji Dk. William, Januari 22, mwaka huu.
Pamoja na mambo mengine, madai yaliyopo katika jalada la kesi hiyo, mlalamikaji Dk. William, ameomba mahakama ikubali Nabii Mwingira apimwe Ukimwi na kipimo cha utambuzi wa vinasaba ‘DNA’.
Nabii huyo amepinga vikali ombi hilo, akieleza kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo (la madai ya kifedha).
MADAI YA MAPENZI
Katika majibu hayo (nakala tunayo), Mwingira amekanusha kufanya mapenzi na mlalamikiwa namba mbili, Dk. Phillis Nyambi ambaye ni mke wa mlalamikaji.
“Mlalamikiwa namba moja amefafanua kuwa hakuingia katika uhusiano wa kimapenzi na mlalamikiwa wa pili,” imeeleza kampuni inayomtetea Mwingira.
AKANA KUBAKA
Nabii huyo pia amekanusha madai ya kumbaka mlalamikiwa wa pili kama alivyosema mlalamikaji katika hati yake ya malalamiko iliyopo mahakamani hapo.
Nabii Mwingira pia amekana madai ya kuzaa na mlalamikiwa namba mbili na kuwepo kwa matatizo ya kitabibu kwa mama huyo ambaye sasa ana mtoto mwenye umri wa miaka mitano, akasema mlalamikaji anatakiwa kuthibitisha.
Kuhusu madai ya Dk. Phillis kushiriki kimapenzi na Mwingira hivyo kusaliti ndoa halali na kumharibia furaha ya maisha mlalamikaji, nabii huyo amesema hajawahi kuwa na uhusiano wowote wa kimapenzi na mwanamke huyo.
Kuhusu madai ya Mwingira kutembea na mke wa mlalamikaji na habari hizo kuandikwa magazetini na kwenye mitandao ya kijamii hivyo kumdhalilisha na kumshushia hadhi, amedai kuwa yeye hahusiki na hilo na atahitaji kuthibitisha.
Madai mengine ya mlalamikaji kwamba vitendo vya walalamikiwa namba moja na namba mbili vya kujihusisha kimapenzi vimemuathiri Dk. Morris kisaikolojia na kiuchumi na kumfanya apoteze biashara zake za kimataifa kwa kukosa wadhamini katika NGO yake, Mwingira amesema kama yametokea hakuyasababisha yeye.
Ameiomba mahakama kuitupilia mbali kesi hiyo na kumuamuru mlalamikaji kulipa gharama za kesi hiyo, hivyo ameweka pingamizi la awali.

Socials