MAPENZI BILA NDOTO NA MALENGO NI WIZI MTUPU,MPENZI MLIYEKUTANA WIKI 2 ZILIZOPITA MKIACHANA HAUTAUMIA KAMA ........

MPENZI uliyeanza naye wiki mbili zilizopita, mkiachana hatakuumiza kama yule uliyedumu naye kwa mapenzi ya dhati kabisa kwa miaka mitatu. Vivyo hivyo, mwandani wako wa miaka mitano halingani machungu na yule wa miaka 10. Yote ni maumivu lakini yanatofautiana. Kwa msingi huo ni kuwa kitambo hutafsiri kiwango cha kuumia. Muongozo huu ukupe sababu ya kukwepa maumivu makali ambayo unaweza kuyapata baadaye. Wote tunakubaliana na msemo wa wahenga wetu kuwa ‘heri nusu shari kuliko shari kamili’.
Maisha ni vile ambavyo wewe mwenyewe unazichanga karata zako. Vilevile unaweza kuyafananisha na mchezo wa bao. Jinsi unavyotumia kete zako kwa mahesabu sahihi na unavyotakata ndivyo unavyokaribisha ushindi.
Kama ukishika kete unawahi kulala, ushindi utausikilizia kwenye bomba. Vilevile maisha ni sawa tu matokeo ya mchezo wa soka, kwa maana kuwa timu iliyosajili vizuri, ikawa na mikakati bora kabisa ya ushindi lazima itashinda.
Pamoja na kulitambua hilo, kwa upande mwingine ni vema ukajua kwamba mapenzi ni kama bangi. Bila shaka utakuwa unajua au umeshawahi kusikia jinsi bangi hufanya kazi ikishaingia mwilini. Humjaza mhusika hisia na matumaini ya uongo ndiyo maana yanaitwa madawa ya kulevya.
Kadhalika mapenzi yanapomlevya mtu hayana tofauti na madawa ya kulevya. Aliyelewa mapenzi si rahisi kujua kama anadanganywa. Hii ni sababu ya wengi kurusha ngumi pale wanapotonywa kuhusu kupigwa changa la macho na wapenzi wao.
Kwanza usikubali mapenzi ya kulevye. Unaruhusiwa kupenda lakini siyo kulewa. Mtu aliyelewa mapenzi hufanya mambo bila kufikiri sawasawa. Je, hujaona mtu anagombana na wazazi kwa sababu ya mpenzi wake? Hiyo ni sehemu ya matokeo ya kulewa.
Nimegusia kote huko ili kutaka utambue kwamba unaweza kusimamia ndoto zako na kuzibaini za mwenzake ikiwa tu utakuwa hujalewa mapenzi. Mtu aliyebwia madawa ya kulevya hana uwezo wa kujidhibiti, hatakuwa na uwezo wa kufanya uamuzi sahihi.
Mbwia unga anaitwa teja, kwa maana hiyo na wewe ambaye mapenzi yatakuingia kama bangi, jina linalokufaa ni teja wa mapenzi. Kwa maana kuwa yatakupumbaza nawe utapumbazika, siku ya kuachwa ndiyo utalia kwa kusaga meno. Usisahau kuhusu wale waliojiua!
Zingatia kuwa mapenzi yatakufanya uwe shujaa, mwenye furaha, matumaini, tena utaonekana mtu bora sana pale yanapokuendea chanya, kinyume chake utachekwa, utakosa furaha na matumaini, tena utaonekana wa ovyo kabisa.
Je, ni sahihi kwako kuonekana wa ovyo? Uchekwe na kugeuzwa mfano wa vijiweni wa watu walioangukia pua katika mapenzi? Bila shaka hutaki hayo yakutokee, kwa hiyo msingi utakaokubeba ni ndoto zenu. Jiulize, wewe na yeye mna ndoto za kuwa pamoja?
Jiulize tena, wewe unaamini kwamba maisha yapo ndani yake na yeye anaamini wewe ndiye maisha yake? Ni mpenzi wa shida na raha au ni wa msimu wa mavuno pekee?

Socials