Internet ikitumika vema inaweza kuleta faida kwa mtu mmoja mmoja. Ukiacha kukusaidia kuburudika na kuwa karibu na watu, kuna faida nyingine kubwa ya kuboresha ufahamu wako ili uweze kuwa mpambanaji hodari wa changamoto mbalimbali za maisha.
Jionee hapa :-
1. Yale yasiyowezekana : Kusoma kunaibua ufahamu wa mambo mengi ambayo pengine ulidhani hayawezekani. Mfano, kama ulidhani si rahisi kuwa mtu wa maisha ya furaha katika mahusiano, baadhi ya makala unazoweza kusoma mtandaoni zitakuonyesha njia zinazoweza kukusaidia kutambua mbinu za kuboresha uwezo wako wa mawasiliano, uwezo wako wa utambuzi wa mahusiano bora na utajikuta unajua uanze wapi. Mfano mwingine unaweza kudhani kuwa wewe hauwezi kuwa na kuendesha blogu, ila baada ya kusoma makala fulani hapa mtandaoni ukajikuta unaweza kuwa na blogu ‘kali’ sana.
2. Mambo yanabadilika: Mengi unayodhani yapo sahihi , pengine hayapo sahihi kwa sasa. Pia mazingira, ufahamu wa watu wengine, teknolojia, hali ya uchumi na kisiasa zinabadilika kwa kasi sana. Hii inaathiri ufanisi wa asasi mbalimbali, na hata ufanisi na ushindani wako katika soko la ajira na ujasiriamali kwa ujumla. Bila kujiboresha mara kwa mara katika kujifunza mambo mapya, unaweza kujikuta upo nyuma ya wakati.
3. Fursa mpya: Mabadiliko na maendeleo yanayoendelea kutokea yanaleta fursa mpya zaidi kwa kila mmoja wetu. Kujisomea kwako kutakuwezesha kutambua fursa husika, na njia sahihi za kuzitumia. Mfano, wajasiriamali wengi wameweza kujitangaza sasa kupitia Facebook kwa kufungua Facebook Fan Page. Hata hivyo, wachache walioweza kujifunza kwa undani namna bora za kutumia pages hizo ndio wamenufaika, wakati wengine pages zimekuwa kama ‘mapambo’ tuu.
4.Fursa zaidi: Hata kama unadhani umefanikiwa sana kimaisha, haina maana kuwa hauwezi kufanikiwa zaidi. Hata kama unadhani una kiwango cha elimu cha kutosha, bado waweza jifunza na kuongeza fursa nyingi za kimaisha, hata kama si kwako binafsi bali kwa wengine wanaokutegemea. Kuna fursa za kuongeza mtandao wako, fursa za kufanya biashara zaidi, fursa za ajira bora zaidi n.k. Haya yanawezekana kwa kuboresha ufahamu wako siku hadi siku.
5. Ufumbuzi wa matatizo: Usikae na tatizo kimya kimya, au ukategemea tuu watu wengine wakutafutie ufumbuzi wa tatizo, liwe la kijasiriamali, la kikazi, la kimapenzi, na hata kidarasani. Tumia vyanzo mbalimbali vya ufahamu hapa mtandaoni kujua mengi yanayoweza kukupa mwanga wa ufumbuzi wa matatizo yako.
6. Uhuru wa fikra: Kuna makala nyingi kutoka kwa asasi na watu binafsi ambazo zinaeleza namna unavyoweza kuwa huru kifkra. Vile ambavyo unaweza kutumia utashi wako kwa ufasaha, bila kuogopa watu wengine. Utaweza pia kujifunza namna bora ya kufanya maamuzi kwa sababu za msingi sio tuu kukurupuka, au kufanya kwa kupendeza watu.