MATUKIO YALIVYOTIKISA NA KUZUA GUMZO 2013.

Rais Barack Obama na mkewe Michelle wakipokea mashada ya maua mara baada ya kuwasili nchini










Zimebaki siku chache kabla ya kuuaga mwaka 2013, mwaka ambao umekuwa na matukio mengi yaliyoitikisa nchi ya Tanzania, huku mengine yakiipa sifa kubwa.
Historia ya Tanzania kuwa na Katiba Mpya itakayopatikana kutokana na maoni ya wananchi ilianza Desemba 31, 2011 wakati Rais Jakaya Kikwete akilihutubia taifa, alikiri wazi kuwa sasa inahitajika Katiba Mpya ili kuendana na wakati wa sasa.
Baadaye Rais Kikwete aliwateua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba na ilianza kazi yake ya miezi 18, kuanzia Mei 3, mwaka 2012.
Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi nchi nzima na kuandaa rasimu ya kwanza ya Katiba ambayo iliitoa Juni 4, mwaka huu.
Baada ya kutolewa kwa rasimu hiyo wananchi walipewa muda wa kuipitia na kuitolea maoni katika Mabaraza ya Katiba ya wilaya, yaliyokaa kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2, mwaka huu.
Maoni hayo yalikusanywa na tume hiyo kwa ajili ya kuyachambua na kutoa rasimu ya pili ya Katiba ambayo inatarajiwa kutolewa Desemba 30, mwaka huu.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitakiwa kumaliza kazi ya kuandaa rasimu ya pili Desemba 15, mwaka huu, lakini Rais Kikwete aliiongezea siku 14 zaidi na hivyo kuifanya iweze kuendelea na kazi hadi Desemba 30.
Hatua hiyo ya Rais Kikwete kuiongezea muda tume hiyo ilikuwa ya pili, kwani mara ya kwanza tume hiyo iliomba kuongezewa muda wa siku 45, kuanzia Novemba Mosi hadi Desemba 15, mwaka huu.
Kabla ya kuomba kuongezewa muda mara ya kwanza, tume ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba 30.
Kwa uamuzi wake, wa kuiongezea Tume hiyo siku nyingine 14, Rais Kikwete ameiongezea tume hiyo jumla ya siku 59 kati ya 60 ambazo anaruhusiwa kisheria.
Kifo cha Dk Sengondo Mvungi
Hatua  ya Rais kuiongezea muda Tume ya Mabadiliko ya Katiba  ilitafsiriwa kama kutoa fursa kwa wajumbe wa tume hiyo kujipanga upya baada ya kifo cha mmoja wa wajumbe wa tume hiyo, Dk Sengondo Mvungi aliyefariki dunia Novemba 12, mwaka huu nchini Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa baada ya kujeruhiwa kwa mapanga na watu wanaotuhumiwa kuwa majambazi, nyumbani kwake mkoani Dar es Salaam.

Socials